Hatimaye mke mdogo wa Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, ameibuka na kujibu baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake yeye binafsi na kwa mume wake na zaidi akisema yote yanayosemwa dhidi yao hayako katika fikra zao kwani kwa sasa baada ya kuachana na siasa wanajipanga kuelekea upande mwingine wa kuwa wawekezaji.
Akizungumza na gazeti la mtanzania jana, Mushumbusi aliitaja mipango yao hiyo kuwa ni pamoja na kujenga shule na hospitali.
Mushumbusi
ametoa kauli hiyo wakati ambapo gharama zinazokadiriwa kufikia shilingi
milioni 50 alizozitumia mume wake katika mkutano wake na waandishi wa
habari mapema wiki hii zikizua mjadala mpana wa alikopata fedha hizo
zote.
Pamoja
na hilo, Mushumbusi ambaye anatajwa kuwa katikati ya mpango wa
kumrubuni mume wake licha ya kupuuza hoja kama hizo alipoulizwa
walikopata fedha za kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo alisema zimetoka
kwa watu aliodai kuwa ni marafiki zao na kiasi kingine ni asilimia 20
ya vipato vyao ambavyo walikuwa wakiviweka kwa muda mrefu.
Mushumbusi
ambaye tangu Dk. Slaa azungumze na waandishi wa habari Jumanne wiki hii
hajawahi kuzungumza lolote, alianza kujibu yale yaliyozungumzwa na mke
mwenzake ambaye ni mke wa ndoa wa Dk Slaa aitwae Rose Kamili ambaye juzi
alizungumza na vyombo vya habari na kumtupia tuhuma nzito yeye
(Mushumbusi) na mume wake huyo wa zamani.
Rose
alikaririwa na vyombo vya habari akimtuhumu mumewe kuwa ni muongo na
anapelekeshwa na mwanamke anayeishi naye kwa sasa ambaye ni Mushumbusi.
Akijibu shutuma hizo, Mushumbusi alisema yeye ni zaidi ya siasa rahisi zinazoenezwa dhidi yake.
Alimpuuza
Rose kwa kusema kuwa ameamua kuchanganya matatizo binafsi ya familia na
propaganda za kisiasa, hivyo jambo hilo liko mbali na uwezo wa fikra na
mipango yake kwa sasa.
Mushumbusi
alisema yeye si mwanasiasa kwani ana mambo mengi anayoyafanya mbali na
siasa hivyo shutuma alizotoa Rose kwa Dk. Slaa zingefaa pia kama
angewaeleza Watanzania sababu za kuachwa kwake.
“I’m
above with that cheap politics, you know? (Unajua niko juu ya siasa
hizo rahisi?), I’m activist, I can’t deal with them and I have a lot of
things to do out of politics by the way, I’m not a politician as I told
you (mimi ni mwanaharakati, siwezi kushughulika nao na nina mambo mengi
ya kufanya nje ya siasa, hata hivyo mimi sio mwanasiasa kama
nilivyokueleza),” alisema Mushumbusi.
Mushumbusi
alifafanua kuwa hivi sasa yuko mbali na mambo ya siasa na anaangalia
mbele kulisaidia taifa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.
Alisema mipango yao kwa sasa ni kujenga shule, hospitali pamoja na kuwasaidia kina mama katika masuala ya ujasiriamali.
Alisema tayari mipango yao hiyo mipya ilikwishapangwa kwa kushirikiana na Dk. Slaa.
Alisema mbali na fedha za marafiki yeye ni mfanyabiashara wa nafaka na kwa muda mrefu pamoja na mumewe wamekuwa wakiweka akiba.
Hata
hivyo, wakati Mushumbusi akisema kuwa anafanya biashara ya nafaka,
gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA) liliwahi kumkariri hivi karibuni
akidai kuwa kwa sasa anafanya biashara ya mkaa.
“Brother
I’m not there as they think, I’m a focused woman (Kaka sipo hapo kama
wanavyofikiri, mimi ni mwanamke makini), nina mambo mengi ya kulifanyia
taifa langu, nashangaa hata hiyo hoja ya kutelekeza watoto, waulizeni
hao watoto kama hawapajui kwangu, huyo kijana wa kiume kila mara anakuja
kwangu hata wadogo zake wanamfahamu vyema, eti wanasema Dk. Slaa
kawatelekeza wanataka awafanyie nini na wakati watoto wote hao ni above
eighteen (zaidi ya miaka 18) na tayari wamezaa kila mmoja, hoja nyingine
you must think big (kufikiri zaidi),” alisema Mushumbusi.
Kuhusishwa na Kinana, Lukuvi
Akijibu
madai ya kutuhumiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, William
Lukuvi ili kumpa maelekezo mumewe juu ya nini afanye baada ya kujiengua
Chadema, Mushumbusi alikana madai hayo kwa kusema kuwa hana mawasiliano
yoyote na watu hao.
“Sina
mawasiliano na Kinana wala Lukuvi kwanza ni watu ambao sijawahi
kufikiria hata siku moja kama nitazungumza nao, kwanza simpendi huyo
Kinana,” alisema Mushumbusi.
Dk. Mwakyembe na Dk. Slaa
Kuhusu
kukutana na Dk. Mwakyembe katika moja ya vyumba vya Hoteli ya Serena
akiwa yeye na mume wake, Mushumbusi alikana taarifa hizo.
Hata
hivyo, gazeti la mtanzania linafahamu kuwa Mushumbusi alikuwepo
katika moja ya vyumba vya hoteli hiyo ambavyo mume wake alivitumia
kukutana na Mwakyembe saa chache kabla ya kuzungumza na waandishi wa
habari.
Pamoja
na ukweli huo, Mushumbusi alisema hana mawasiliano na Mwakyembe ingawa
alikiri mume wake kukutana naye ili kupata ufafanuzi wa baadhi ya hoja
za sakata la Richmond.
“Dk
alihitaji kupata ufafanuzi fulani wa hoja za Richmond, kumbuka ripoti
ya Richmond iliandikwa kisheria zaidi hivyo alimuhitaji Dk. Mwakyembe
kwa ajili ya kupewa ufafanuzi wa baadhi ya vipengele ndipo walipokutana
saa chache kabla ya mkutano na wanahabari,” alisema.
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment