Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi CCM na mgombea ubunge Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema CCM haijakamilika kwa asilima 100 na kwamba kuna mambo machache ambayo hayako sawa lakini wanayafanyia kazi.

Nape amesema bianafsi anaupenda sana upinzani wa vyama vya siasa hapa nchini kwa kuwa wamekuwa wakiishtua Serikali ya CCM kwenye mambo machache ambayo yamekuwa yakilala ama kwenda kinyume na utaratibu.

Nape aliyasema hayo jana wakati akizindua Kampeni ya “Nimeshtuka” ambayo inawahusisha wasanii mbalimbali ambao awali walikuwa wanachama wa Chadema na kumuunga mkono mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowasa ambapo kwa sasa wasanii hao wamehamia CCM.

Katika mkutano huo, Nape alibeza uamuzi wa Lowassa kuhamia Ukawa na kuongeza kuwa CCM imejipanga kushinda uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.

Alienda mbali zaidi na kuwaomba wananchi kumuombea dua Lowassa aweze kuwa na afya njema ili Oktoba 25 aweze kushuhudia ushindi wanaoupata CCM.

Kwa upande wake kiongozi wa wasanii hao ambao wamejitoa Ukawa, Vincent Kigosi maarufu kwa jina la Ray alisema kuwa walipokwenda Ukawa walidhani wanakwenda kwenye safari ya matumaini hata hivyo baadaye waligundua safari hiyo haikuwa ya matumaini.

“Nimezunguka na Lowassa baadhi ya maeneo lakini sijaona sera za maana na zenye mashiko, nawaambia vijana wenzangu mimi nimeshtuka na nyie hebu shtukeni” amesema Kigosi.

Naye msanii wa filamu, Aunt Ezekiel aLIwataka vijana kujituma kwa kufanya kazi kwani hakuna mtu anayeweza kuwapa mabadiliko ya maendeleo isipokuwa ni vijana wenyewe.

ALIwashauri vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuichagua CCM badala ya kufuata mkumbo kwa kuamini ahadi zisizotekelezeka.

Wasanii wengine waliokuwemo kwenye Kampeni hiyo ni pamoja na Juma Nature, Inspekta Haroun ‘babu’, Kitale na wengine.

Post a Comment