Serikali
imesema itasambaza mabomba ya gesi nchi nzima ikibidi hadi nje ya nchi
na kuiuza ili kujenga uchumi imara huku ikiahidi kuandaa mpango mkakati
utakaowashirikisha wadau wakiwemo Ewura kuhakikisha bei ya umeme wa gesi
inashuka ili watanzania wote waweze kunufaika na huduma hiyo.
Hayo yamesemwa na waziri wa nishati na madini Mh, George
Simbachawene alipotembelea kituo cha uzalishaji wa umeme Ubungo namba
mbili jijini Dar es Salaam kuona mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi
iliyowashwa na shirika la umeme nchini Tanesco ambapo tayari megawati 90
zimekwishaingia kwenye gridi ya taifa.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika la umeme nchini
Tanesco injinia Felshesm Mramba amesema mitambo iliyowashwa inazalisha
umeme wa gesi kutoka Mtwara vizuri na hakuna hitilafu, mushkeri, wala
dosari yeyote.
Uwekezaji wa mradi wa umeme wa gesi kutoka Mtwara kuja Kinyerezi
hadi katika mitambo ya Ubungo jijini Dar es Salaam ni mkubwa kuliko yote
nchini umegharimu kiasi cha dola bilioni 1.22 na utamaliza tatizo la
mgawo wa umeme nchini sambamba na kupunguza gharama kubwa kwa Tanesco
kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vya maji, mafuta mazito na mepesi
ambapo kwa mujibu wa serikali licha ya kuwa na mpango mkubwa wa kujenga
megawati 600 kwa mikoa ya kusini Lindi na Mtwara kwa kuanzia imesema
kitaalamu itapeleka megawati 20 ndani ya miezi miwili ili kumaliza
kabisa tatizo la umeme kwenye mikoa hiyo kunakotokea gesi hiyo.
Post a Comment