Polisi Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wamesusia posho
zilizotolewa baada ya kukamilisha kazi ya kusimamia mitihani ya darasa
la saba waliyoifanya hivi karibuni.
Taarifa kutoka wilayani humo zinaeleza kuwa askari hao wamechukua
uamzi huo kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa mabadiliko ya kiwango
cha posho walizotakiwa kupewa kwa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa askari aliyenukuliwa na gazeti la Mwananchi,
walitarajia kupewa posho ya shilingi 65,000 kwa siku lakini walijikuta
wakitakiwa kusaini shilingi 22,500 tu kwa siku.
Aidha, katika baadhi ya halmashauri, polisi wamelipwa shilingi 40,000
kwa siku kwa ajili ya kazi hiyo, kiwango ambacho bado ni pungufu ya
kile kilichokuwa kimepangwa.
Akizungumzia madai hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Fulgence Ngonyani aliwaambia waandishi wa habari kuwa viwango hivyo
vilipangwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na kwamba vilitofautiana
kulingana na majukumu ya kazi husika.
“Waliosimamia vituo teule ambavyo ndivyo vinahifadhi mitihani, na
wale wanaosindikiza walilipwa posho shilingi 40,000,” alisema Kamanda
Ngonyani. “Na wale waliosimamia tu walipata 22,500,” aliongeza.
Post a Comment