Fukuto lililojitokeza ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi baada ya
Katibu Mkuu pamoja na mwenyekiti msaidizi wa chama hicho kutangaza
kutoridhishwa na mwenendo wa mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi kupitia
Ukawa, limepelekea kuwepo taarifa za tishio la kumuangamiza mwenyekiti
wa chama hicho, James Mbatia.
Taarifa za kuwepo kwa njama za kutaka kumuangamiza Mbatia zilitolewa
jana na mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi ambaye pia ni
mkuu wa idara ya Sheria, Haki za Binadamu na Katiba, Mohamed
Tibanyendera.
Alieleza kuwa idara ya usalama ya chama hicho imepata taarifa za
kiintelijensia kuhusu kuwepo njama za kumdhuru mwenyekiti wa chama hicho
katika mkutano wa hadhara wa kampeni.
“Chama kimepokea taarifa kutoka idara ya usalama kuwa kuna watu
wameandaliwa kuleta machafuko. Watavaa sare katika kampeni zinazoendelea
na watavamia na kupiga viongozi, mlengwa mkuu ni Mbatia,” alisema
Tibanyendera na kueleza kuwa chama hicho kimeziamini taarifa hizo kwa
namna zilivyowasilishwa.
Alieleza kuwa Mbatia alishauriwa kufikisha taarifa za tishio hilo kwa
jeshi la polisi na alifanya hivyo kwa kuwasilisha maelezo ya kuwepo
tishio hilo katika makao makuu ya jeshi la polisi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na mwandishi wa gazeti la
Mtanzania, msemaji mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alipotaulizwa
aliwataka wana habari kumuamini James Mbatia bila kutoa ufafanuzi wa
moja kwa moja kama tayari jeshi hilo limeshapata taarifa hizo kutoka kwa
Mbatia.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi anadaiwa kutopokea simu tangu taarifa hizo ziliporipotiwa.
Post a Comment