Sidhani kama kuna ubaya kwa watu wanaopenda kufuatilia siasa na mienendo ya kampeni kujumuika katika mikutano mbalimbali kuwasikiliza wagombea nyadhifa za uongozi katika maeneo yao na nchi nzima kwa ujumla.
Nadhani ni njia sahihi ya kuweza kuwasikia wagombea kuendana na eneo na
tukio husika, kuliko kusubiri kusikiliza vipande tu kupitia vyombo
mbalimbali rasmi na visivyo rasmi vya habari.
Ili watu waweze kuhudhuria mikutano hiyo kwa wingi, bila shaka ni sahihi
kabisa kutumia vyombo vya usafiri kwa mtu binafsi au kama kundi, ili
kurahisisha shughuli nzima.
Linalonitatiza katika mwenendo huu, ni hili la Serikali kupiga marufuku
mara kadhaa usafirishaji watu na abiria kwa kutumia vyombo visivyo rasmi
kwa usafiri wa abiria kama vile magari ya kubebea mizigo na wanyama.
Agizo la kusitisha mara moja kubeba abiria kwa kutumia vyombo hivi
lilitolewa hasa baada ya kutokea ajali huko Dodoma, Mbeya na Arusha.
Iweje lifumbiwe macho katika nyakati hizi za kampeni ambapo watu
wanakuwa wamejaa mhemuko na mshawasha wa kisiasa kiasi cha kuwa kama
waliorukwa na akili?
Tutasubiri mpaka ajali itokee ndipo tuseme, "Mapenzi ya Mungu" na kuomba
walazwe pema wakati tulishaumizwa nayo na tunaiona hatari yake wakati
huu?
Post a Comment