Pichani ni Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini NCCR Mohamed Tibanyendera  akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.Picha: Karoli Visenti.


SIKU moja kupita baada ya Makamu mwenyekiti wa chama cha NCCR-mageuzi, Reticia Mosore pamoja Katibu Mkuu wa chama hicho John Mwambabe kuibuka na kumtuhumu Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia kukiua chama chao kwa kile wanachodai kuwa wamepewa majimbo machache ya uchaguzi,Chama hicho kimeibuka na kusema wanasikitika na viongozi hao kubadilika dakika hizi za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu kwani hatua zote za ugawaji wa majimbo hayo viongozi hao walishiriki kwenye hatua zote.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini NCCR Mohamed Tibanyendera amejibu malalamiko hayo kwa kusema Chama hicho kimesikitishwa  na kauli za viongozi hao kipindi hiki cha mwisho kwani maamuzi yote yaliyofikiwa na UKAWA yalifuata kanuni zote na kwamba hata ofisi ya Katibu mkuu huyo ndio ilikuwa inahusika katika majimbo hayo
 
“Sisi NCCR tunashangaa kwa kauli za Katibu wetu pamoja na  Makamu mwenyekiti kwani kipindi majimbo yagawiwa kwenye vyama, Ofisi ya Katibu ilikuwepo na ndio ilikuwa inapanga majimbo hayo.
 
"Ugawaji wa majimbo ulizingatia ushindani wa kisiasa pamoja na nguvu ya eneo husika. Wote kwa pamoja tulikubaliana na hali hiyo, sasa tunashangaa leo wanakuja kubadilika” amesema Tibanyendera
 
Amesema Majimbo 22 walioyopata NCCR kwa upande wa Ukawa ni mengi sana ukizingatia na miaka ya nyuma
 
“Jamani NCCR tumekaa zaidi ya miaka 10 bila hata kuwa na mbunge hata mmoja, 2010 tukapata wabunge 4 tu wakuchagulia,sasa leo kupitia ukawa,NCCR imesimamisha wabunge 22 kupitia majimbo tofauti nchini maana yake ni zaidi ya mara 5 ya wabunge tuliopata sasa, huku wabunge wetu 4 waliopo wanaendelea kugombania” amesema
 
Tibanyendera ameongeza kuwa madai  wanayotoa yalitakiwa kutolewa kwenye vikao halali vya chama hicho  kwa mujibu wa katiba ya chama.

Tibanyendera amedai kuwa viongozi hao walikuwepo kwenye kikao kikuu kilichofanyika tarehe 16 mwezi huu, na suala hilo wanalodai hawakulizungumia kwenye kikao hicho lakini wanashangaa leo kuibuka mbele ya vyombo vya Habari  na kutoa lawama kwa mwenyekiti .
 
Aidha,Tibanyendera amewataka Wanachama vya Vyama vinavyounda UKAWA ambavyo ni Chadema,Cuf na NLD kupuuza madai ya viongozi hao na kuyachukulia ni watu binafsi na sio ya chama ,akidai kuwa NCCR itaendelea kuwa sehemu ya UKAWA na kitakuwa chama cha mwisho kujitoa ukawa.
 
Amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya Octoba 25 mwaka huu na kumchagua mgombea wa Urais kupitia umoja huo Edward Lowassa pamoja na wabunge na madiwani wanaounda Ukawa.

Post a Comment