Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC jaji mstaafu Damian Lubuva amevitaka vyombo vya habari nchini kutenda haki kwa kutokuegemea upande wowote kwani wakitumia kalamu zao vibaya zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.


Jaji Lubuva ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wamiliki wa vyombo vya habari ambapo amesema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki kwani matokeo yote yatabandikwa katika vituo vya kupigia kura hadi ya urais tofauti na miaka mingine ambapo matokeo ya urais yalikuwa hayabandikwi.
 
Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa vyombo vya habari MOAT Dk Regnald Mengi amesema kuna umuhimu wa tume hiyo kuboresha utoaji elimu kwa mpiga kura kwa kuchapisha habari nyingi kwa lugha rahisi na kuitaka tume kukemea uvunjifu wa maadili unaofanywa na wanasiasa.
 
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa uchaguzi NEC Bw Emanuel kawishe amesema vyombo vya habari vitaruhusiwa kurusha matokeo ya urais moja kwa moja na kuongeza kuwa kampeni za uchaguzi katika majimbo na kata zilizoahirishwa zitaanza Octoba 13 mwaka huu lakini Octoba 25 na 26 zitasitishwa kwa ajili ya kupisha zoezi la kupiga na kuhesabu kura.
 
Mkurugenzi utangazaji TCRA Bw Habi Gunze mbali na kuvipongeza vyombo vya habari hasa luninga na radio kwa kufuata kanuni za uchaguzi, ameitaka NEC kuweka bayana kituo maalum cha kutolea matokeo ya kura kwani vyombo vya habari haviwezi kufika kila kituo nchini.
 

Post a Comment