Wenger Ashindwa Kumjibu Mourinho

Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekataa kujibu kadhia zilizotolewa na meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho ambazo alizitoa mwishoni mwa juma lililopita alipokutana na vyombo vya habari kuelekea katika mchezo dhidi ya Newcastle Utd uliomalizika kwa matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili.


Wenger alikataa kujibu lolote lililoulizwa na waandishi wa habari kuhusu tuhuma alizotupiwa na Mourinho, kwa madai aliushinikiza uongozi wa FA kumuadhibu mshambuliaji Diego Costa baada ya mchezo wa September 19 ambapo Chelsea waliwafunga Arsenal mabao mawili kwa moja.

Wenger, aliwataka waandishi wa habari kuachana na maswali yaliyotokana na kauli za meneja huyo kutoka nchini Ureno na badala yake alitaka kuulizwa kuhusu mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita ambao ulimalizika kwa Arsenal kupata ushindi wa mabao matano kwa mawili dhidi ya Leicester City.

Mourinho alimchimba Arsene Wenger kwa kusema mzee huyo wa kirafansa ameridhika na maisha ya kujiachia akiwa Arsenal kwa kuamini hatokufukuzwa kutokana na udhaifu wake, na sasa ameanza kufuatilia mambo ya watu kwa kushinikiza viongozi wa soka kutoa adhabu dhidi ya wachezaji wa timu pinzani.
Mourinho amejenga tabia ya kumrushia madongo Arsene Wenger kwa kutumia kigezo cha babu huyo kushindwa kutwaa ubingwa wa nchini England kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini kwa bahati mbaya amekua akikosa majibu ya kejeli kutoka upande wa pili

Post a Comment