Mwenyekiti mwenza wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia ameomba kufanyika mdahalo kati
ya vyama vinavyounda umoja huo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbatia alitoa ombi hilo jana usiku katika mkutano na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam ambapo aliwasihi viongozi wa CCM kuwachagua
wasemaji wao ili waweze kujumuika pamoja katika mdahalo kwa lengo la
kunadi sera na ilani za vyama vyao.
“Tunawataka CCM wachague msemaji wao, na kwa kuwa Ukawa haitambuliki
kama chama cha siasa, vyama vyote vya upinzani vitaweka wasemaje wao,
ili tuache porojo na maneno maneno,” alisema Mbatia na kuongeza kuwa
vyama ndivyo vinavyowakilisha mfumo wa serikali inayotarajiwa na sio mtu
mmoja.
Kadhalika, Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi alizungumzia
taarifa zilizoeleza kuwa mgombea wa Chadema aliomba kura kanisani.
Alisema habari hizo ni za uongo kwa kuwa Lowassa aliwaomba waumini wa
dini yake kumuombea na sio kumpigia kura. Alisema Lowassa sio mshirikina
na ndio sababu amemtanguliza Mungu kwenye kampeni zake.
Aidha, alieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) walipaswa
kumkemea mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa kauli yake kuwa mabadiliko
yanaweza kuisababishia nchi matatizo kama ya Libya. Alisema badala ya
kumkemea NEC iliwaeleza kuwa kauli hiyo ni ‘vionjo vya kisiasa’. Alisema
kauli hiyo haikuwa kauli ya busara kwa kuwa ililenga katika
kuwashawishi wananchi kwa kuwatishia hali ya usalama.
Katika hatua nyingine, Mbatia alimkosoa mgombea urais wa CCM kwa kile
alichodai kuwa anataka kujitenganisha chama chake ili aonekane kuwa
yeye sio chama katika kukwepa kubeba majukumu ya maswali ya watanzania
kwa chama hicho.
“CCM ni Magufuli na Magufuli ni CCM, watanzania msirubunike,” alisema
Mbatia akitoa mfano wa mabango ya mgombea huyo kuwa hivi sasa
yameandikwa ‘Chagua Magufuli’ huku yakikitenga chama tofauti na miaka
iliyopita ambapo wananchi walihimizwa kuchagua Chama sio mtu.
Post a Comment