Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema maana na neno M4C, linalotumiwa na Chadema ni "Magufuli for Change” akimaanisha ndiye atakayeleta mabadiliko.
Dk
Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika Kata ya Nguruka, Jimbo la Kigoma
Kusini mkoani Kigoma, alipohutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ambapo
aliwabeza wapinzani kuwa hawawezi kurudi kwa wananchi kuangalia shida
zao.
“Mkiangalia
hizi picha za wagombea, mimi nimevaa shati, mwingine amevaa suti. Sasa
huyu mwenye suti anaweza kukubali kuja kupata shida na nyinyi huku?” alihoji na kuongeza:
“Wanasema M4C, mnajua maana yake?” aliuliza mgombea huyo na kujibu mwenyewe, “maana yake ni ‘Magufuli for Change’.
Katika
mkutano huo, mgombea huyo alimtaka mgombea ubunge wa chama hicho katika
jimbo hilo, Hasna Mwilima amwachie matatizo ya jimbo hilo
ayashughulikie mwenyewe.
Matatizo
yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo ni bei ya tumbaku, kukosekana kwa
umeme na maji na upandishaji hadhi kituo cha afya cha Nguruka kuwa
hospitali ya Wilaya ya Uvinza.
Dk
Magufuli alisema kazi ya kwanza atakayompa waziri wake wa kilimo,
itakuwa ni kutafuta soko la zao la tumbaku kwa mikoa ya Tabora na Kigoma
ili wananchi wauze kwa bei nzuri.
“Mchagueni
Hasna Mwilima ili akawawakilishe bungeni, lakini kwa matatizo haya
niachieni mimi. Haiwezekani mpaka sasa Nguruka hamna umeme,” alisema mgombea huyo.
Akiwa
katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, alimtambulisha mgombea ubunge wa
jimbo hilo, Peter Serukamba na kuwataka wananchi kumchagua ili
akashirikiane na Serikali yake bungeni.
Lakini
ilipofika zamu ya mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Dk Amani
Kabourou, hali ilibadilika na kutokea minong’ono ya wananchi kama ishara
ya kumkataa pale alipopewa nafasi ya kuwasalimia.
Dk
Kabourou alianza kuzungumzia mipango yake endapo atachaguliwa kuwa
mbunge wa jimbo hilo kwa mara nyingine, hata hivyo wananchi walisikika
wakisema ‘hapana, hapana’ huku wakinyoosha mikono juu kuonyesha ishara
ya kumkataa mgombea huyo.
Wakati
Dk Magufuli alipojaribu kumnadi mgombea huyo, wananchi walianza tena
kupiga kelele, wakisema ‘hatumtaki...’ jambo lililomfanya Dk Magufuli
kutomwombea kura na kuendelea kuzungumzia mambo mengine.
Post a Comment