Mlinda mlango tegemeo wa Real Madrid kwa sasa, Keylor Navas amefichua siri ya uchungu aliouhisi baada ya kuambiwa na viongozi wa klabu hiyo hatoweza kujiunga na Man Utd.

 

Navas, ameelezea siri hiyo kutokana na matarajio aliyokua amejiwekea ya kuelekea nchini England kujiunga na Man Utd, kama sehemu ya kubadilishana na David De Gea ambaye alikua mbioni kurejea nyumbani mjini Madrid mwishoni mwa mwezi uliopita.

Navas amesema alikua na ndoto za kuitumikia klabu ya Man Utd katika maisha yake na aliamini kama angefanikiwa kuelekea Old Trafford, msimu huu angethubutu kucheza katika kikosi cha kwanza.
Amesema tayari alikua ameshakata tamaa ya kuendelea kubaki Real Madrid kutokana na ufinyu wa kucheza kila juma, na ujio wa De Gea ambao ulikua unapewa msikumo mkubwa klabuni hapo, ulimchanganya kabisa kwa kuona mambo yangeendelea kumuharibikia.

Hata hivyo kwa sasa Navas amesisitiza kuwa na furaha huko Estadio Stantiago Bernabeu, kutokana na kupata nafasi ya kucheza kila juma na anaamini ataendelea kudumu hapo kama ilivyokua kwa walinda milango wengine waliomtangulia.

Navas mwenye umri wa miaka 28, alikua na wakati mgumu wa kucheza tangu aliposajiliwa klabuni hapo mara baada ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 akitokea Levante UD, kutokana na ushindani uliokua unamkabili kutoka kwa Iker Casillas Fernández aliyetimkia FC Porto mwanzoni mwa msimu huu.
Navas alionyesha kiwango kizuri wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka jana zilizofanyika nchini Brazil akiwa na timu ya taifa lake la Costa Rica.

Post a Comment