Serikali
ya awamu ya tano ya chama cha mapinduzi CCM imewahakikishia wananchi wa
mkoa wa Mara ambao sehemu kubwa umezungukwa na migodi ya madini kuwa
itahakikisha wawekezaji kwenye migodi hiyo wanachangia maendeleo ya
wananchi wa maeneo husika sanjari na kukuza pato la taifa kupitia
maliasili zilizopo nchini endapo wananchi wataipa ridhaa ya kuliongoza
taifa.
Mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM Dr John Pombe Magufuli ambaye
amefanya mikutano minne katika maeneo ya Nyamongo, Tarime, Rorya,
Musoma vijijini na hatimae Musoma mjini kwenye uwanja wa Mkendo ambapo
ameendelea kusisitiza kauli yake ya maendeleo hayana chama na kuahidi
kutatua kero mbalimbali kulingana na maeneo alikopita na kusisitiza kuwa
serikali yake haitakuwa na msalie mtume kwa mafisadi, wezi, na wazembe
ili mwananchi wa kawaida aweze kupata faraja ya kuwa mtanzania.
Kuhusiana na suala la maliasili za taifa hususani madini Dr
Magufuli amesema serikali yake inawakaribisha wawekezaji wa nje na wa
ndani kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la ajira na kukuza uchumi
lakini kamwe hatakubali Tanzania kugeuzwa shamba la bibi.
Dr Magufuli anahitimisha ziara yake mkoani Mara ambapo aliwasili
akitokea mkoani Tanga na kuzuru kaburi la baba wa taifa hayati Mwl
Julius Kambarage Nyerere na baadae kukabidhiwa na wazee wa eneo la
Butiama kifimbo kama cha baba wa taifa kama ishara ya kiongozi ama
mtawala anayekubalika na anatarajiwa kuendelea na ziara yake mkoani
Simiyu jumamosi sept 12.
Post a Comment