Maxmillian Rafael Msacky (wapili kushoto) na Patrick James Natala (wa tatu kulia)  wakiwa mahakama ya kisutu jana Ijumaa.

Watu wawili, Patrick Natala na Maxmillian Msacky wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo ya kughushi, kutengeneza tovuti feki na mifumo ya mtandao kwa kutumia majina ya Taasisi, viongozi na wanasiasa.

Akiwasomea hati ya mashtaka jana Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa akishirikiana na Wakili Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura walidai kuwa washtakiwa hao walitengeneza tovuti feki kwa kutumia majina ya Taasisi ya Jakaya Kikwete Foundation (Ikulu), TCRA Foundation, Akiba Saccos Social Company, Social Credit and Loans Company, Ridhiwani Social Company, Hisa Tanzania, Zitto Kabwe Foundation, Vicoba Tanzania na Wekeza Fund.

Mutakyawa alidai kuwa washtakiwa hao wametengeneza tovuti hizo feki kati ya Januari na Aprili 2014 jijini Dar es Salaam kinyume na kifungu cha 122 (b) cha sheria ya Kielektoliniki na Mawasiliano ya Posta namba 3 ya 2010.

Mbali na mashtaka hayo, Mshtakiwa Msacky yeye anadaiwa kuwa kati ya 2006 na 2024 kwa njia ya udanganyifu alighushi cheti cha Sekondari namba 0421130 chenye indexi namba S 0260-0001.

Iliendelea kudaiwa kuwa kati ya 2005 na 2014 mshtakiwa huyo alighushi cheti kingine cha Sekondari namba 0217951 chenye indexi namba S 0310-0532,akionyesha ni halali na kwamba vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania wakati akijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa hao walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa walipelekwa rumande hadi Septemba 28, 2015 itakapotajwa.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Sheria wa TCRA, Elizabeth Nzage alisema kati ya Aprili na Juni katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 walipata malalamiko toka kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa makampuni feki yaliyokuwa yakidai kuwa yanatoa mikopo kwa muda mfupi.

Nzage alidai kuwa wahusika hao walitumia majina ya wanasiasa na pia kujifanya ni viongozi na wamiliki wa taasisi hizo na kwamba makumpuni hayo yanaandaa shughuli za kuchangisha fedha.

Post a Comment