Makamu
wa rais Dk Mohamed Gharib Bilal amewaongoza waombolezaji kuuaga mwili
wa aliyekuwa waziri wa nchi, ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa
umma Mh Celine Kombani zoezi lililofanyika viwanja vya Kareemje jijini
Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa maziko.
Mara baada ya mwili huo kuwasili katika viwanja hivyo mchungaji
Wilfred Mmari ameongoza ibada fupi ya kumuombea marehemu kabla ya
makundi mbalimbali kutoa salaam zao za rambirambi.
Akisoma salamu za serikali waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu
sera, uratibu na bunge Mh Jenista Mhagama mbali na kueleza uadilifu
uliotukuka wa marehemu Kombani amesema ndani ya serikali ameacha pengo
huku mwakilishi wa serikali ya mapinduzi Zanzibar naye akitoa salaam.
Naye spika wa bunge anayemaliza muda wake Mh Anne Makinda akitoa
salaam kwa niaba ya ofisi ya bunge amewataka watumishi wa umma kutumia
msiba huo kutafakari na kurekebisha maisha yao kwa kuwa na upendo na
kuwatumikia wananchi kwa kutoa huduma bora.
Baadhi ya mawaziri wenzake na wabunge waliojitokeza kuuaga mwili
huo wamemwelezea marehemu Kombani namna alivyokuwa mwalimu wao kila mara
walipotaka ushauri wake ndani na nje ya bunge.
Mbali na makamu wa rais baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria
zoezi hilo ni pamoja na mawaziri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa,
mama Maria Nyerere na mama Salma Kikwete.
Akisoma wasifu wa marehemu mwakilishi wa serikali amesema marehemu
alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya kongosho iliyokuwa
imeathiri ini lake na alizaliwa june 19 1959 na kufarifariki dunia
septemba 24 mwaka huu katika hospitali ya Apollo nchini India na mwili
wake unatarajiwa kuzikwa sept 29 mkoani Morogoro na ameacha mume,watoto
watano na wajukuu wanne.
Post a Comment