HALI si shwari! Mjengo wa staa wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ uliopo Kimara Saranga, Dar ambao alisema amemzawadia mama yake mzazi, Lucresia Karugila, umezua utata baada ya madai kwamba eti umeshauzwa.


Kwa mujibu wa chanzo ambacho ni jirani mmoja wa eneo hilo, mjengo huo umeuzwa kutokana na uamuzi wa Lulu mwenyewe bila kujulikana sababu licha ya manenomaneno kwamba, mama Lulu alikuwa hataki kuhamia hapo akitaka mjengo mkubwa zaidi kama wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ uliopo Madale, Dar.

Jirani huyo alisema kuwa, ni muda mrefu hajamwona Lulu wala mama yake licha ya kwamba kuna mlinzi wa kulinda nyumba hiyo lakini anaishi nyumba nyingine ya jirani.

“Watu wanasema umeshauzwa, lakini mnunuzi hajajulikana. Ila mtu ambaye anaweza kuwaambia kwa undani zaidi ni Lulu mwenyewe. Yule mlinzi hayuko wazi sana. Ila nyumba imeisha kwa sasa,” alisema jirani huyo akiomba jina lake liingizwe kwenye ghala.

Baada ya kupata ubuyu huo bila kupoteza muda mapaparazi wetu walifunga safari mpaka Saranga kwenda kujiridhisha na kile walichoelezwa na sosi huyo na kushuhudia mjengo huo wa maana ukionekana upo tayari mtu kuweza kuishi lakini kukiwa hakuna mtu ndani.

Wakazi wa eneo hilo walihoji siku ambayo mama huyo atahamia kwenye mjengo wake huo aliozawadiwa na mwanaye huku wengine wakidai walipata fununu nyumba hiyo imeshapigwa bei.

“Hakuna kitu cha kumkwamisha kuhamia kwa sababu bado madirisha tu ndiyo hayajakamilika japo tayari kuna magrili, sasa nashangaa mbona hawahamii na isitoshe hakuna hata mlinzi. Mtu si anaweza kuingia akawa analala bila ridhaa yao!

“Kuna kipindi Lulu alikuwa anakuja hapa na mama yake kuitazama lakini baadaye akawa anakuja mama yake tu japo kipindi hiki cha karibuni tangu nyumba ifikie hatua hiyo ya kuisha sijawaona wote,” alisema mmoja wa majirani zake.

Baada ya hapo, mapaparazi wetu walimvutia ‘waya’ mama Lulu na kumsomea madai yote ambapo alijibu kwa kifupi:

“Jamani naomba mniache kwanza, si mnajua nimetoka kufiwa siku si nyingi. Hivyo bado akili yangu haijakaa sawa kwa pigo nililolipata. Hayo mambo siwezi kuyaongelea kwa sasa.”

Baada ya hapo, mapaparazi walimsaka Lulu kwa njia ya simu na alipopatikana alikuwa na haya ya kusema:

“Hizo ni ishu binafsi za kifamilia, siwezi kuzizungumzia sana kama nikitaka kumkabidhi mama nitamuita ndani na kumkabidhi, nikitaka kuanika kwenye vyombo vya habari nitasema, ila mengine hayo siyajui.”

Post a Comment