Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ameponda kauli ya vyama vya upinzani kuwa vitaleta mabadiliko, akisema kazi hiyo tayari imefanywa na CCM.

Akizungumza kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Bukoba wakati wa uzinduzi wa kampeini za wagombea wa chama hicho mkoani Kagera, Mkapa alisema chama pekee kilichobobea katika ukombozi ni CCM na Serikali zake zilizotangulia.
 
Kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu alisema kuwa lengo la vyama vya upinzani ni kuing’oa CCM na lengo la chama hicho tawala ni kuendelea kushika dola, hivyo upinzani unatakiwa kujifunza hadi baada ya miaka 50.

Alitaja miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa awamu tofauti kuwa ndiyo aina ya mabadiliko ya maendeleo wanayohitaji wananchi, akitaja uwanja wa ndege wa Bukoba na barabara za lami.

“Hayo ndiyo mabadiliko ya maisha ya Watanzania huwezi kuleta ajira kwa kutamka tu, tulianzisha wilaya na mikoa mipya ili kuchochea maendeleo ya wananchi na maisha yao hayo ndiyo mabadiliko,’’ alisema Mkapa.

Jana, alionekana kuzungumza kwa tahadhari kwa kile alichodai akiwaeleza wapinzani ukweli wanadai ana jeuri.
 
Hata hivyo, katika hotuba yake alishindwa kujizuia na kutamka neno mbumbumbu na kusema hataki kuwazungumzia.

Kabla ya kumkaribisha Mkapa kuhutubia, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye alisema wagombea wote wamepita kwenye mchujo sahihi na kutamba kwamba chama hicho kimejipanga kupata ushindi.

Post a Comment