Askofu Josephat Gwajima amejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa kuwa alishiriki kama
‘mshenga’ kumshawishi mwanasiasa huyo kumpokea Edward Lowassa katika
chama hicho.
Jana, Dk. Slaa alimtaja Askofu Gwajima kama mshenga na kwamba
alimshawishi ampokee Lowassa huku akidai kuwa askofu huyo alimtamkia
kuwa maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki walihongwa na timu ya Lowassa.
Askofu Gwajima amekanusha taarifa zilizotolewa na Dk. Slaa ambaye
alikuwa rafiki yake kwa muda mrefu akidai kuwa ni muongo mkubwa. Alisema
kuwa Dk. Slaa ameamua kuwashambulia maaskofu hao kwa kuwa anafahamu
hawana majukwaa ya kumjibu kama ilivyo kwa wanasiasa.
Gwajima alidai kuwa yeye aliitwa kama msuluhishi ndani ya Chadema na sio mshenga wa kumleta Edward Lowassa.
“Kwa kawaida inashangaza kwamba kama watu wawili wanagombana
inatakiwa awepo mtu wa kuwaunganisha, ila anaposema maaskofu 34 haileti
maana, haiingii akili, ameingiza Gwajima, Rostam Aziz na maaskfu,”
Gwajima ameliambia gazeti la Mtanzania na kuongeza kuwa Dk. Slaa
ametumwa na watu anaowafanyia kazi.
Askofu huyo alidai kuwa alichokisema jana Dk. Slaa kilikuwa silaha
pekee ya CCM iliyokuwa imebaki na kuwataka waumini wake na watanzania
kutoamini alichosema mwanasiasa huyo.
“Nafikiri Slaa ndio risasi ya mwisho ya mwisho iliyokuwa imebaki kwenye bunduki ya CCM,” alisema.
Jana Dk. Slaa alitangaza kustaafu siasa za vyama akieleza kutokana na
kutoridhishwa na mwenendo wa siasa nchini hususani Chadema aliyoijenga
kwa ajenda ya kupinga ufisadi na badala yake wamemkumbatia Lowassa
waliyekuwa wanamtuhumu kuwa fisadi mkubwa.
Post a Comment