Aliyekuwa Katibu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ametoa majibu ya
baadhi ya maswali yanayoulizwa na wananchi baada ya hotuba yake
iliyomshambulia kwa tuhuma za ufisadi Edward Lowassa na chama hicho.
Akiongea katika mazungumzo maalum na Azam TV, Dk Slaa ameelezea
kuhusu suala la alikotoa fedha za kugharamia matangazo ya televisheni na
ukumbi wa hotel ya kitalii ya ‘Serena’.
Dk. Slaa amekiri kuwa tukio hilo liligharamiwa na watu wengine japo
hakuwataja watu hao, na kudai kuwa hiyo sio mara ya kwanza watu wengine
kumgharamia.
“Kwanza nawashangaa, hivi mwaka juzi, mwaka jana nimeenda Marekani
sikuulizwa hizo gharama,” alisema na kudai kuwa Chadema hawakuwahi
kugharamia ziara yake nchini Marekani na kuwataka watoe vielelezo kama
waliwahi kufanya hivyo.
“Waweke hadharani senti hata moja ya chama kulipia safari ya Dk. Slaa
Marekani,” alisema. Hata hivyo alibainisha kuwa chama hicho kilimlipia
shilingi laki tano kwa ajili ya kuandaa nyaraka alizoendanazo Marekani.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa ambaye alitangaza kustaafu siasa,
alikanusha habari zilizoenea kuwa amekimbia nchi kuelekea nchini Canada,
mara baada ya kutoa hotuba yake.
“Wanasema sipo tena Tanzania, nilishaondoka toka tarehe ile
nilipomaliza press conference tu, lakini mimi niko hapa na wewe tuko
Azam studio, kwa hiyo unaweza ukaona aina ya upotoshwaji uliokuwepo,”
alibainisha.
Dk. Slaa anadaiwa kutumiwa na Chama Cha Mapinduzi kudhoofisha kampeni
za urais za Ukawa na kwamba chama hicho tawala kilimuandalia mkutano
huo na waandishi wa habari pamoja na gharama za kurusha matangazo ya
Televisheni zinazokariwa kuwa zaidi ya milioni 89.
Madai yanayotolewa na baadhi ya uongozi wa Ukawa yalieleza kuwa Dk
Slaa anachuki na hasira ya kunyimwa nafasi ya kugombea urais kupitia
umoja huo, nafasi aliyopewa Edward Lowassa aliyepokelewa na Chadema
akitokea CCM.
Post a Comment