YANGA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk. Jonas Tiboroha, imesema
wapo tayari kumwachia kocha msaidizi wao, Charles Boniface Mkwasa,
kukitumikia kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, ikilitaka Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) kufuata utaratibu.
TFF wapo katika mpango wa kumpa Mkwasa mkataba wa kudumu baada ya
kuridhishwa na maendeleo ya Stars tangu kuondoka kwa Mholanzi, Mart
Nooij, japo hajashinda mechi hata moja kati ya tatu walizocheza.
“Tupo tayari kumwachia, TFF wafuate utaratibu wa kuvunja mkataba,
ana mkataba na sisi wa miaka miwili ambao ameutumikia kwa miezi minane
tu,” alisema Tiboroha.
TFF chini ya Rais Jamal Malinzi, walimteua Mkwasa kukaimu nafasi ya
Kocha Mkuu wa Stars kwa muda wa miezi mitatu, muda ambao unaelekea
kufikia ukingoni.
Mkwasa alijikuta akizidi kujiongezea sifa baada ya wapenzi wa soka
nchini kuishuhudia Stars ikicheza soka la hali ya juu dhidi ya Nigeria
juzi na kutoka nayo suluhu.
Mchezo huo ulikuwa ni wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon 2017) zitakazofanyika nchini Gabon.
Post a Comment