Hofu imetanda juu ya moyo wa ‘Ninja’ kutoka Tanga, Roma Mkatoliki
masaa machache baada ya kuachia wimbo wake mpya alioupa jina la ‘Viva’.
Rapa huyo anahofia wimbo wake kufungiwa muda wowote kwa madai kuwa
ameanza kupokea taarifa za kufungiwa wimbo huo ambao umerusha makombora
mazito yanayogusa sehemu ambazo zimewafanya hata mashabiki wake kuhofia
hatma ya wimbo huo.
Akiongea na Jabir Saleh katika kipindi cha The Jump Off cha 100.5
Times Fm jana usiku, Roma alisema kuwa sio mara ya kwanza watu kuhofia
kupokea nyimbo zake kutokana na mashairi mazito anayoyaandika. “Hakuna
aliyenituma, nimetumwa na wananchi niwaongelee na nilichoongea ni ukweli
mtupu,” alisema Roma huku akitetea baadhi ya mitari tata iliyoko kwenye
wimbo huo.
Aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi, mashabiki wake
walikuwa wanasubiri kwa hamu kusikia anasema kitu kuhusu kile
kinachoendelea hivyo alitumia muda mwingi kuandika kile alichokiita
ukweli mtupu.
Akielezea nini kitatokea endapo wimbo wake utafungiwa, Roma alisema
kuwa ingawa uamuzi huo utaathiri harakati zake lakini anaamini ujumbe
wake utafika.
“Hata wakati ule nilipotoa wimbo wa Mr. President, kuna baadhi ya
radio ulikuwa ukienda unakuta kabisa ‘memo’ kuwa wimbo huo usichezwe
kabisa. Lakini wimbo ulihit mitaani tu hivyo hivyo,” alisema.
Alieleza kuwa wimbo wake wa Mathematics ulifanya vizuri zaidi ya
nyimbo zake zote zilizopita kwa sababu tu uliruhusiwa kuchezwa radioni
bila vipingamizi na sio kwamba ndio ulikuwa wimbo mkubwa zaidi.
Post a Comment