Mgombea ubunge wa jimbo la Bunda mjini kwa tiketi ya Chadema,
Ester Bulaya juzi alimuokoa mtoto wa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa
tiketi ya CCM, Stephen Wasira aliyekuwa anataka kuchomwa moto na
wananchi.
Kwa mujibu wa Ester Bulaya, mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la
Kambarage alitaka kuchomwa moto katika kata ya Kunzugu eneo la Bukore
kwa madai ya kukamatwa na wananchi hao akigawa rushwa kwa baadhi ya
vijana ili waweze kufanya fujo kwenye mkutano wa mgombea huo uliopangwa
kufanyika katika eneo hilo hivi karibuni.
Akiongea na waandishi wa habari jana, Bi. Bulaya amesema kuwa alipata
taarifa kuwa wananchi wamewafungia ndani ya nyumba makada kadhaa wa CCM
akiwemo mtoto wa Wasira na aliamua kuwachukua askari wa jeshi la polisi
na kuwahi katika eneo la tukio ambapo waliwakuta watu hao.
“Jana (Juzi) mtoto wa Wasira na wenzake tumewaokoa wakitaka kuchomwa
moto ndani na wananchi ambao walipata taarifa zao za kukutana ili wawape
watu rushwa waje kufanya fujo kwenye mkutano wangu ninaopanga kuufanya
Bukore,” alieleza Ester Bulaya.
Mgombea huyo alivitaka vyombo vya usalama na wagombea kwa pamoja
kukemea vitendo hivyo vya rushwa vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa
amani.
Kwa upande wa Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) Wilaya ya Bunda, Alex Mpenda alikiri kutokea kwa tukio hilo
na kudai kuwa alifika kwenye eneo la tukio na kukuta watu hao
wameshaondolewa na jeshi la polisi.
Post a Comment