Njia mpya ya kutia dawa za kuua mbu kwenye vyandarua imefanikiwa kwa asilimia 100 katika kukabili baadhi ya aina za mbu, ripoti ya utafiti wa kimataifa inasema.
Njia hiyo inayotumia nguvu za umeme za elektrostatiki kupaka dawa huwezesha vyandarua kubeba viwango vya juu vya dawa.
Wakati wa kufanyiwa majaribio, dawa iliyotiwa kwenye vyandarua kwa njia hiyo, ambayo kwa Kiingereza inajulikana kama electrostatic coating, iliua mbu wengi kuliko kawaida.Watafiti kutoka Uholanzi, wakiandika kwenye jarida la afya la Proceedings of the National Academy of Sciences, wamesema njia hiyo inaweza kusaidia kukabili baadhi ya magonjwa kama vile Malaria.

Mbu kuzoea dawa limekuwa tatizo sugu katika maeneo mengi yanayotatizwa na malaria duniani.
Inadhaniwa dawa za maji za kunyunyizwa pamoja na neti za vitanda, ambazo mara nyingi huwa na viwango vya chini vya dawa, huwa mara nyingi haziui mbu, na kuwafanya kuzoea dawa.





Kwenye utafiti wa sasa, watafiti kutoka Uholanzi, walitumia sehemu yenye nguvu za umeme, iliyotayarishwa awali kwa kunasa chavua hewani, na kuipaka dawa.

Kutumiwa kwa nguvu za umeme aina ya electrostatic zinazodumu muda mrefu kuliwezesha viwango vya juu vya dawa kujishikilia upesi na vyema kwenye vyandarua, na kuhakikisha mbu wanapata dawa ya kutosha kuwaua wanapogusa neti - hata kama ni sekunde chache tu.

Mbinu hiyo ilifanyiwa majaribio kwenye aina tofauti tofauti za mbu Afrika Kusini, Tanzania na kwenye maabara ya kitivo cha dawa za maeneo yenye mvua nyingi cha Liverpool.

Watafiti walibaini kuweka dawa kwa kutumia nguvu hizo za umeme kuliwezesha kuuawa kwa mbu wengi, ikilinganishwa na neti zilizopakwa dawa kwa njia nyingine na kwa baadhi ya mbu ambao wamekuwa hawasikii dawa, ilifanikiwa asilimia 100.
Neti za kawaida huua chini ya asilimia 10 ya mbu, utafiti huo ulisema.
aliyeongoza utafiti huo, kutoka In2Care, katika Chuo Kikuu cha Wageningen, nchini Uholanzi, amesema njia hiyo ya kupaka dawa inaweza kutumiwa kwenye vitambaa vya kufunika madirisha na milango nyumbani, na kwenye mitego ya mbu na mashimo ya kupitishia hewa manyumbani.

"Ni njia mpya ya kulenga kuwafikia na kuwapa dawa mbu," amesema.
Aidha, amesema njia hiyo mpya itafaa sana kwani inaweza kutumiwa na aina mbalimbali za dawa.

Hata hivyo, amesema njia hiyo ya kupaka dawa huenda haifai kwa neti za kufunika vitanda kwani watu huzigusa mara kwa mara na kwa hivyo dawa hiyo inaweza kutoka baada ya muda.

Post a Comment