Wananchi katika jimbo la Karatu wamekosoa uamuzi wa aliyekuwa
mbunge wa jimbo hilo, Dk Slaa kumshambulia mgombea urais kwa tiketi ya
Chadema Edward Lowassa.
Wakazi hao wa Karatu wamemkataa Dk Slaa kwa kudai kuwa uamuzi
aliouchukua hausaidii katika harakati za kuikondoa CCM madarakani bali
inazirudisha nyuma juhudi hizo.
Kwa mujibu wa The Citizen, wananchi waliofanya mahojiano kwa nyakati
tofauti wameeleza kuwa hawatabadili msimamo wa kuiunga mkono ngome ya
Ukawa kama alivyotaka Dk Slaa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi
cha miaka 15 tangu mwaka 1995.
“Ni bora tuwe na mafisadi wachache walioko upinzani kuliko kuwa na
mafisadi zaidi ya 100 ambao bado CCM inawakumbatia,” alisema Isack
Philip, mkazi wa kata ya Rhotia, Karatu.
Wananchi wengine walifika mbali kwa kuonesha jinsi wasivyounga mkono
CCM wakidai wako tayari hata kuchagua jiwe badala ya chama hicho tawala.
“Tuko radhi kuchagua jiwe badala ya CCM ambayo tangu tupate uhuru
imekuwa ikituangusha katika kupata maendeleo,” alisema muendesha
bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Emanuel Bayo na kuongeza kuwa
madai ya Dk Slaa hayana mashiko wakati huu.
Wananchi wengi waliofikiwa na gazeti hilo walieleza kuwa nia yao ni
kuhakikisha wanaona CCM ikiondolewa madarakani na sio vinginevyo.
Hata hivyo, mwenyekiti wa zamani wa CCM katika wilaya hiyo, alimtetea
Dk Slaa na kueleza kuwa anatoa mawazo na mtazamo wake kwa lengo la
kuwaonesha watanzania hali halisi.
Hivi karibuni, Dk Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema alijitokeza
hadharani na kupinga uamuzi wa chadema kumpokea Edward Lowassa na kumpa
nafasi ya kugombea urais licha ya kukiri kuwa yeye ndiye aliyelipeleka
wazo hilo kwa uongozi wa chama chake ambacho kilikuwa kimemteua yeye
kugombea nafasi hiyo.
Post a Comment