Jeshi la kujenga taifa JKT limesema linaendelea na harakati za kuboresha mazingira ya mafunzo kwa vijana wa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya mafunzo vinavyojumuisha sare pamoja na viatu ili kuyafanya mafunzo hayo kuwa bora na yenye kuwajenga vijana katika moyo wa uzalendo kwa nchi yao.

Mkuu wa jeshi la kujenga taifa JKT.Meja Jenerali Raphael Muhunga amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya JKT kwa vijana wa mujibu wa sheria yaliyopewa jina la oparesheni Kikwete mwaka 2015 katika kambi ya mafunzo ya kikosi cha jeshi cha 841 Mafinga mkoani Iringa na kueleza kuwa lengo la kushughulikia changamoto hizo za vifaa vya mafunzo ni kuboresha mafunzo hayo ili yalete tija zaidi kwa taifa na wahitimu wenyewe.
 
Katika risala yao wahitimu hao wapatao zaidi ya elfu wamesema moja ya changamoto zilizowakabili katika muda wote wa mafunzo ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kujifunzia ikiwemo buti na kombati pamoja na muda wa mafunzo kuwa mfupi hali iliyowalazimu kufanya mafunzo yao katika mazingira magumu huku wakikabiliwa na mambo mengi ya kujifunza katika muda huo mfupi ambapo mkuu wa kambi ya jeshi hilo kikosi cha 841 Mafinga luteni kanali Martin Mkisi amewapongeza wakufunzi wa mafunzo hayo kwa uvumilivu na ubunifu.
 
Ufungaji wa mafunzo hayo umeambatana na maonesho mbalimbali ya vijana hao wahitimu walioonesha ukakamavu na ustadi walioupata mafunzoni ikiwemo kucheza kwata, kuchoma singe kucheza karate na kuruka vikwazo maonesho yaliyodhihirisha jinsi vijana hao walivyoiva kimafunzo.
 

Post a Comment