skofu wa Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima jana
alijibu tuhuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa
ambaye siku chache zilizopita alimtaja askofu huyo kama mshenga
aliyempeleka Edward Lowassa katika chama hicho.
Katika hotuba yake, Dk Slaa alimtaja askofu huyo kuwa ndiye
aliyemwambia kuwa maaskofu 30 kati ya 34 wa kanisa katoliki walihongwa
fedha na Edward Lowassa.
Akiongea na waandishi wa habari, Gwajima alijibu mapigo kwa kueleza
siri nyingi kati ya wawili hao huku akidai kuwa Dk Slaa ni muongo na
kwamba aliudanganya umma kwa shinikizo la mkewe aliyenunuliwa na maadui
wa Chadema. Alisema mkewe huyo tayari alikuwa amejiandaa kuwa ‘first
lady’ na hakutaka kupoteza nafasi hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Gwajima alieleza kuwa Dk Slaa aliudanganya
umma kuwa sababu za yeye kuachana na siasa ni ujio wa Edward Lowassa
ndani ya Chadema iliyokuwa ikipinga ufisadi. Alidai kuwa Dk Slaa ambaye
alikiri ni rafiki yake, ndiye aliyemfuata na kumshawishi ampeleke
Lowassa Chadema ili awezeshe chama hicho kushinda katika uchaguzi mkuu.
“Dk. Slaa alikuja kwangu nimuunganishe na rafiki yangu Lowassa kwa
sababu ni mtu mwenye mvuto katika chama chake, jamii na ana nguvu
kisiasa. Mimi nataka nikiri kwamba nilifanya kila linawezekana ili
kuhakikisha Lowassa anakwenda Chadema,” alisema.
“Dk. Slaa alivyoniita Mshenga hakukosea kwa sababu ninajua kila kitu.
Mimi kusaidia kumleta Lowassa Chadema ni kazi ya Mungu, maana Biblia
inasema ‘heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu’.” Aliongeza.
Gwajima alieleza kuwa Dk Slaa alikuwa na nia ya kumpeleka Lowassa
Chadema akiwa kama Katibu Mkuu wa Chama na kwamba ndiye aliyemkutanisha
na mwenyekiti wa chama hicho na mwisho kuingia katika kamati kuu ambapo
alipokelewa vizuri na wananchama wa chama hicho baada ya kuhutubia.
Alisema hata hivyo mke wa Dk Slaa, Josephin aligeuka kikwazo kikubwa
baada na kuanzisha ugomvi akimtaka kubadili mawazo yake, huku akisimulia
tukio la kutupiwa begi nje na mkewe na kulazimika kulala kwenye gari
lake.
Gwajima alisema walinzi wa Dk Slaa ambao alipewa na askofu huyo miaka
mitano iliyopita ndio walimfahamisha kuhusu tukio hilo la kulazwa nje.
Pia, Dk. Slaa alimtumia ujumbe ambao aliuonesha kwa vyombo vya habari,
ujumbe uliokuwa ukieleza kuwa Dk Slaa anataka kuachana na siasa kwa kuwa
familia yake inapasuka.
Katika hatua nyingine, Gwajima amemuelezea mke wa Dk Slaa kuwa ni mtu
mwenye mashetani na mara nyingi amekuwa akimuombea na kwamba ameibadili
akili ya Dk Slaa na kusema hayo anayoyasema leo. Alisisitiza kuwa
kinachoongea sio akili ya Dk Slaa, bali anaendeshwa na mkewe.
Aidha, alikanusha kauli ya Dk Slaa kuwa alimwambia maaskofu
walihongwa na wakagawana fedha mbele ya macho yake. Alimtaka kuacha mara
moja kuwahusisha maaskofu na siasa kwa kuwa anachokizungumza sio kweli
na kwamba anapaswa kuacha uongo unaowachafua maaskofu ili kumridhisha
mtu au chama kilichomtuma.
Baada ya maelezo marefu, Gwajima alimuonya Dk Slaa kutorudia kumtaja
kwa kuwa siri zake zote anazifahamu na kwamba alikuwa anarekodi maongezi
yao.
“Nasema kama Dk. Slaa atajaribu kujibu haya, nitatoa siri nzito namna
alivyokwenda Afrika Kusini akiwa na wanne wanne pamoja na mzigo uliopo
na mahali ulipotunzwa,” alisema.
Wakati Gwajima anatoa maelezo hayo, taarifa zinaeleza kuwa Dk.
Wilbroad Slaa amesafiri na familia yake kuelekea nchini Marekani. Hata
hivyo, Dk Slaa ameiambia Azam TV kuwa ameondoka nchini sio kwa kukimbia
bali ameenda kwa ajili ya mapumzika na atakuwa akifuatilia
kinachoendelea nchini.
Haijafahamika kama bomu hilo la Gwajima limepokelewaje na Dk Slaa, na
kama atajitokeza tena kujibu huku kukiwa na onyo la askofu huyo ambaye
amewataka maaskofu wote kutohangaika na tuhuma za Dk Slaa kwa kuwa yeye
atammudu.
Post a Comment