CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kitashinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa sababu kina mtandao mkubwa wa wanachama kuanzia ngazi ya chini na kwamba kufurika kwa wananchi katika mikutano ya Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa sio ushindi, kikisema kura ni mahesabu.

Aidha, kimesema kuwa mgombea huyo wa Chadema na umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), amedanganywa na wapambe wake kuihama CCM na kumkejeli ikisema gari la wagonjwa linapaswa kuwekwa nyumbani kwake siku ya uchaguzi kwani CCM itapata ushindi wa uhakika asubuhi.

Akitoa taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisisitiza kuwa ushindi wa chama hicho tawala na kikongwe hauna shaka kutokana na mtandao wake kuanzia ngazi ya chini.

Akijibu swali kuhusu kufurika kwa wananchi katika mikutano ya mgombea huyo wa Chadema, Nape alisema: 
 
“Kwa walioanza siasa jana ndio watashituka. Mwaka 2010 Slaa (Dk Willibrod) katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni Mbeya alipata watu wengi kuliko wale aliopata Edward. Lakini kura alizopata Mbeya utashangaa. 
 
“Kupata watu wengi mkutanoni hakutushangazi kwani kura ni mahesabu, hawa (Chadema na mgombea wao) wanatoka pointi moja kwenda nyingine. CCM ina mtandao, ukiondoka mjumbe wa nyumba kumi anapitia watu wake anasafisha nyayo zenu,” alisema kiongozi huyo.

Nape aliongeza kuwa wapinzani wote wametoka ndani ya CCM kuanzia kwa Augustino Mrema mwaka 1995 na hadi katika chaguzi nyingine zilizofuta na zote wapinzani walishindwa, na hata safari hii CCM itashinda.

Akimgeukia Lowassa, Nape alisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu, amedanganywa na wapambe wake na kuondoka chama tawala, na kwamba licha ya kuhamia huko, CCM itamshinda asubuhi na kuwataka wanaotishia kukihama kufanya hivyo na si kuleta shinikizo.

“Katika mchakato wa uchaguzi si wote watakaoridhika na matokeo kwa sababu kuna wengi wanajiandaa kushinda na sio kushindwa, na matokeo yanapokuwa hivyo, wanakuwa hawaridhiki na hapo ndipo wanazungumzia kwenda upande wa pili, na hasa kwa shinikizo la wapambe.

“Hili limetokea kwa Edward, amekwenda upande wa pili, amedanganywa na watu, tutampiga. Ushindi wa CCM ni wa uhakika, sio wa matumaini. Matumaini yapo Angaza, CCM ni ya uhakika. Tutashinda asubuhi. Tumesema ni mpambano kati ya wagombea na makapi,” alisema Nape na kuongeza: 
 
“Zipo mechi ambazo unajua hii utashinda. Yanga na Lipuli ya Iringa unajua matokeo yake. Tunataka mgombea mwenzetu apelekewe ambulance (gari la wagonjwa) nyumbani kwake, kwani ushindi kwetu ni uhakika.
 
” Kuhusu wanaolalamika na kutishia kuhama, alisema malalamiko hayawezi kutolewa barabarani kwani chama hicho kina utaratibu wake na yale yote yaliyolalamikiwa yakiwamo ya udiwani, yamefanyiwa kazi.
 
 “Tulisema wakati ule wa mchakato wa kutafuta mgombea wa urais kuwa hatutafanya kazi kwa shinikizo. Tunajua uimara wa chama chetu, kama kuna watu wanataka kwenda upande wa pili waende. Lakini CCM haiwezi kufanya kazi kwa vitisho na shinikizo. 
 
"Tatizo ni kwamba kunatokea wagombea 12, halafu unasema lazima uwe wewe. Kuna watu (wanaotaka kuhama) wanafanya hivyo kwa shinikizo la viroba na hela,” alisema Nape.

Post a Comment