Viongozi
wa dini, taasisi zisizokuwa za kiserikali na vyama vya siasa vimelitaka
jeshi la polisi na tume za taifa za uchaguzi NEC na ZEC kutenda haki na
kuwa wawazi kwa kila jambo ambalo wananchi na wadau wanapaswa kujua ili
amani iendelee kudumu wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.
Wakizungumza katika kongamano la amani na utulivu wakati wa
uchaguzi mkuu lililoshirikisha wadau mbalimbali, na kufanyika jijini Dar
es Salaam baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki wamesema amani ni
tunda la haki hivyo kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo kwa
kutenda haki na kuzingatia sheria uchaguzi mkuu utamalizika kwa amani na
utulivu.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nao wakaelezea mambo kadhaa
yanayochangia uvunjifu wa amani hasa wakati wa uchaguzi huku wengine
wakiahidi kuendelea kuonyesha ustahamilivu na ustaarabu wakati wote wa
kampeni ikiwa ni pamoja na kutii sheria bila shuruti na kuvitahadharisha
vyombo vinavyosimamia uchaguzi kutokuhubiri suala la amani midomoni tu
badala yake waonyeshe kwa vitendo kwa kusimamia haki.
Mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa Peter Mzirai amesema
mijadala ya mara kwa mara kuelekea uchaguzi mkuu ndio kiungo muhimu na
kushauri kuundwa kwa kamati ya kupokea migogoro ya vyama vya siasa na
ishughulikiwe kwa wakati huku mkuu wa operesheni na mafunzo wa jeshi la
polisi Paul Chagonja akijibu hoja kadhaa na kuwataka wanasiasa kueleza
sera zao wawapo majukwaani badala ya kuanza kukashfiana.
Akihitimisha kongamano hilo mwakilishi kutoka tume ya uchaguzi
Zanzibar ZEC pamoja na kujibu hoja zilizohusu NEC Bw Ramadhan Omary
Mapuri amesema suala la wanafunzi wa vyuo vikuu watumie fursa ya
kuhakiki majina kwa kwenda kwenye halmashauri au vituo
walivyojiandikishia kubadilisha taarifa zao huku mwakilishi wa MOAT Bw
Henry Muhanika akielezea hatua walizochukuwa katika kutoa elimu kwa
wanahabari.
Post a Comment