CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua kampeni zake jijini Dar es Salaam kwa kuahidi kitakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Aidha
katika uzinduzi huo ambao viongozi mbalimbali wa chama hicho
walihutubia, Mgombea Urais wa chama hicho Anna Mghwira alisema wananchi
wakimpa ridhaa, waziri mkuu wake atakuwa Zitto Kabwe.
“Nitakapounda
serikali, katika katiba, mtu wa kwanza kusaidiana na rais licha ya
makamu, ni Zitto Kabwe, atakuwa Waziri Mkuu katika serikali ya kwanza,”
alisema Anna Mghwira ambaye pia alisema atahusisha viongozi waadilifu
kutoka CCM, Chadema na vyama vyote vya siasa na taasisi zote kiraia.
Akihutubia
mkutano huo uliofanyika viwanja vya Mbagala Zakhem, mgombea huyo,
katika kuelekeza nia yake ya kuunda serikali hiyo ya umoja, alisema
linapokuja suala la kitaifa, hakuna haja ya kuangalia masuala ya
itikadi.
“Mimi
ni mama, hukusanya watoto wake.Hata mama wa vifaranga hukusanya
vifaranga pamoja na kuviweka kwenye mbawa zake…mimi nina mbawa za
moyo…nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayotokana na sekta
binafsi lakini kutoka watu wazalendo, wenye utu, waadilifu, taasisi za
kijamii, mashirika ya kidini, makundi ya umma ili kuunda taswira ya nchi
yetu.”
Mghwira
alisema taifa linahitaji mabadiliko si ya tu kifikra na kisera, bali
pia ya kijinsia kwa kumchagua yeye kuwa Rais wa nchi. Alisema chama
chake kinatilia mkazo utu, uzalendo na uadilifu.
Makao makuu Dodoma
Aidha
alisema, Serikali itakapoundwa itaapishwa Dodoma na watahakikisha
wanarudisha kazi kubwa aliyoifanya Rais wa Kwanza, Julius Nyerere ya
kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na serikali lakini siyo makao
makuu ya chama.
Alisema kuweka mji huo makao makuu, maana yake ni kuleta watu wote kutoka pande zote za nchi.
Vipaumbele
Alitaja
vipaumbele vyake ni kuwa na mfumo imara na endelevu wa hifadhi ya jamii
unaojengea uwezo wananchi kukabiliana na majanga. Alisema asilimia sita
pekee ya Watanzania wanafaidika.
“Tutatumia
hifadhi ya jamii kama nyenzo ya kukuza akiba nchini ili kuwe na vyanzo
vya mitaji ya uwekezaji wa ndani…tutapanua hifadhi ya jamii kufikia
makundi yote katika jamii ikiwamo wakulima, wafugaji, mama lishe na
bodaboda,” alisema.
Kipaumbele kingine alichoahidi ni uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora.
Alisema
watu wengi hawana uhakika na maisha yao kimapato. Aidha alisema,
watajikita kwenye uwekezaji wa kilimo na kusimamia uzalishaji wake.
Aidha,
aliahidi kuhakikisha ardhi na mashamba yote yaliyo chini ya mashirika
ya umma, yanachukuliwa na kuwekwa chini ya uzalishaji mdogo.
Kwa upande wa viwanda, alisema atahakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinaongeza mapato ya fedha za kigeni.
Chama
hicho kupitia kwa mgombea, kimesema kitaweka msukumo kwenye bidhaa za
nguo na vitakuwapo viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na
mifugo.
Vipaumbele vingine ni kuhakikisha madini, mafuta na gesi, vinakuwa mali ya wananchi kikatiba.
Kuhusu
Katiba Mpya, alisema wataruhusu Tume ya Jaji Warioba imalize kazi ya
katiba ilikoishia. Mgombea huyo aliendelea kutaja vipambele vyake
kuhakikisha anaboresha huduma za afya ikiwamo kudhibiti vifo vya mama na
mtoto.
Aliahidi
kuondoa tatizo la watoto wa mitaani. Misamaha ya kodi kwa mujibu wake,
haitazidi asilimia moja ya pato la taifa na wakati huo huo atadhibiti
mianya ya ukwepaji kodi hususani kwa kampuni za kigeni.
Sifa za rais
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo, alishauri wananchi
kuangalia wagombea urais kama wanalinda haki za walio wengi au ni mateka
wa matajiri.
Mkumbo
alisema, kiongozi mkuu wa nchi, kwa maana ya rais, ana kazi kuu nne
ambazo ni fikra na kutoa dira ya nchi jambo ambalo anapaswa kuwa na
uwezo wa kufikiri.
“Tatizo ni kufikiri na kutoa dira ya nchi…tunataka rais atakayetoa misingi ya nchi, atatuletea sera..,” alisema Kitila.
Alisema
kazi ya pili ya rais, ni kuwa mlinzi mkuu wa tunu za taifa huku
akisisitiza katika tunu ya umoja, wananchi kuepuka mgombea mwenye tabia
za kidini, kikabila na kikanda.
“Rais ndiye mlinzi wa usawa katika taifa…,” alisema na kushauri wananchi kuangalia wanaogombea kama wanaelekea kulinda haki za walio wengi au ni mateka wa matajiri.
Alitaja tunu nyingine ni muungano kwa kusema anayeomba urais na kutaka kucheza na muungano lazima akataliwe.
Kuhusu uadilifu, alisema inapaswa aingie rais atakayekoleza vita ya ufisadi . “Kama kuna mtu anataka urais hata kutamka neno ufisadi anaogopa, huyu hatufai hata kidogo,” alisema Kitila.
Akizungumzia
demokrasia, alisema nchi imepiga hatua katika demokrasia ambayo
inahitaji rais atakayeipeleka mbele. Vile vile alisema katika kuchagua,
ni lazima kuangalia mgombea ndani ya chama chake alipatikanaje.
“Kazi
nyingine ya rais lazima awe mfano wa binadamu bora katika jamii.
Hatumaanishi malaika, tunamaanisha kwamba popote atakapoenda, akisimama
wajue huyu ni Mtanzania, awe sura ya utaifa,” alisema na kusisitiza sifa nyingine ya rais itokane na uadilifu wa chama chake.
Kitila alisisitiza,
“Mtu asiye mlaghai lazima aliyotuambia jana, na leo yafanane. Akihubiri
maji lakini yeye anakunywa wiski, yeye ni mlaghai. Akituambia ni nyeusi
jana, leo nyekundu, kesho nyeupe, huyo ni mlaghai.”
Alisisitiza kuwa ACT Wazalendo inazingatia misingi na sera huku akibeza vyama vingine kwamba vinauza mbwembwe na ulaghai.
Ukawa wasutwa
Kwa
upande wake, Meneja wa Kampeni, Habib Mchange, aliisuta Chadema na CUF
kupitia viongozi wao akirejea mkutano wa Mwembe Yanga mwaka 2007,
walipotaja orodha ya waliowatuhumu kuwa mafisadi papa. “Kipindi kile hawakuwa na Ukawa bali walikuwa na ushirikiano.
Walitaja
watu wanaofilisi taifa hili ambao ni watu kumi na moja…kati ya watu hao
waliotajwa kuwa ni mafisadi, namba tisa alikuwa ni Lowassa,” alisema Mchange.
“Tulikubaliana
2007 kwamba tunapambana na CCM na wana mafisadi. Leo naomba
mtafakari…ili tusiwe wajanja wajanja lazima tuseme ukweli.Unayosema jana
ndo hayohayo uyaseme leo,” alisema.
Akinyoshea
CCM pia vidole, Mchange alilinganisha mgombea wa Ukawa sawa na chupa
yenye sumu iliyobandikwa jina la maji. Alinadi chama chake akisisitiza
wananchi wakiamini kwa kuwa kimekuja katikati ya sumu mbili za CCM na
Ukawa.
Amshangaa Sumaye, Lowassa
Mchange alisema anachoona ni kwamba, ufisadi uliokuwa CCM, umezaliana na kutanuka na hatimaye kuhamia Ukawa. “Jana (juzi) Sumaye ametulaghai… Anasema anashangaa kwa nini CCM inaendelea kuaminiwa,” alisema.
Alikumbusha
kuhusu mjadala wa kununua ndege ya rais ambayo ilipigiwa kelele, kwamba
wakati huo Sumaye ndiye alikuwa Waziri Mkuu.
Pia
kuhusu ahadi ya Lowassa ya kumwachia huru mwanamuziki Nguza Viking
maarufu kama Babu Seya, Mchange alieleza kushangazwa naye kutokana na
kile alichosema, wakati anafungwa, ndiye alikuwa Waziri Mkuu.
Mchange alikuwa mkali zaidi katika hotuba yake hasa alipokuwa anazungumzia ufisadi na wizi. “ Kumbe unaruhusiwa kuwaibia Watanzania ukiwa CCM ukirudi upinzani ni msafi. Mwizi ni mwizi tu.
Fisadi ni fisadi tu…Wanatudanganya kwamba kuna Ukawa…waongo. Ukawa wanatafuta rais tu. Ukawa huku chini kwa wapiga kura haupo,” alisema Mchange.
Alihoji
ni namna gani mgombea urais ataweza kunadi wagombea wa vyama
vinavyounda Ukawa ambao wamegoma kuachiana majimbo hususani Jimbo la
Tabora Mjini, Serengeti na Segerea.
“Sasa tuwaulize Ukawa Lowassa akipita Tabora mjini atamnadi nani?,” alisema akimaanisha mgombea wa CUF na Chadema wanaogombea jimbo hilo.
Zitto Kabwe Alisema ACT Wazalendo wanarejesha miiko ya uongozi.
Alisisitiza
kuhusu utaratibu wa chama chake wa kiongozi kutangaza mali na madeni
yake. Zitto alisema kila chama kinachogombea, kinasema kitapambana na
rushwa na ufisadi bila kueleza ni namna gani watapambana tofauti na ACT
Wazalendo ambacho kimesema kitapambana kwa kurejesha miiko ya uongozi.
Alihoji ni namna gani mawaziri wakuu wastaafu wanatamba kuleta mabadiliko.
Zitto
alimsuta Sumaye akisema, wakati ATCL inauzwa aliyekuwa Waziri Mkuu ni
Sumaye na wakati huo huo na mwaka 2007 ilipotaka kufufuliwa wakapewa
Wachina ambao walisababisha hasara kwa taifa aliyekuwa Waziri Mkuu
alikuwa Lowassa.
Zitto
alikosoa pia kauli ya Magufuli juu ya ahadi yake ya kuanzisha mahakama
ya kupambana na rushwa, akisema kwenye katiba mpya, kulikuwa na
kipengele cha kuipa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
mamlaka ya kukamata na kushitaki wala rushwa lakini CCM waliikataa.
Kuhusu
ufisadi, Zitto alisema hakuna chama cha siasa chenye uwezo wa kupambana
nao isipokuwa ACT Wazalendo. Akitumia kete ya jinsi kumnadi mgombea,
Zitto alisema, ni wakati wa Watanzania kumpa mwanamke uongozi wa nchi
ikizingatiwa miaka yote, imekuwa ikiongozwa na wanaume.
Post a Comment