Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hana deni la kulipa kwa mtu yeyote akichaguliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa hakutoa rushwa wakati wa uteuzi ndani ya chama hicho.
Magufuli
alitoa kauli hiyo jana wakati akijinadi yeye na wagombea udiwani na
ubunge wa CCM mkoani Mbeya ili wachaguliwe katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk.
Magufuli alikuwa akijinadi na wagombea hao kwa nyakati tofauti katika
mji wa Mbalizi na wilayani Songwe eneo la Mkwajuni, Makongolosi wilaya
ya Chunya.
Magufuli
ambaye jana alikuwa katika siku ya nne ya kujinadi kwa wananchi na
kuomba kura tangu kufunguliwa kwa pazia la kampeni mikoani, alisema
tangu kuanza kwa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM wa urais ndani ya
chama hicho, hakutumia fedha bali alikwenda kimya kimya makao yao makuu
kuchukua fomu na kuzirejesha.
Alisema kwa mantiki hiyo, hana cha kulipa kwa sababu hadaiwi na mtu yeyote.
Magufuli
alisisitiza kuwa anachofahamu ni kwamba deni kubwa alilonalo ni
kuwatumikia Watazania na kuwaletea maendeleo ili wazidi kuwa na maisha
bora.
“Nilichukua
fomu kimya kimya na kurudisha kimya kimya, natembea na barabara ili
shida zenu ziwe shida zangu, ili nikiingia Ikulu nizishughulikie kwa
haraka,” alisema.
Magufuli
alisema anaamini kuwa kuteuliwa kwake na CCM kupeperusha bendera ya
chama hicho katika kinyang’anyiro hicho kuna makusudi ya Mwenyezi Mungu
ili afanye kazi.
“Sikutoa rushwa kwa kuwa ni dhambi na adui wa haki... niliacha mchakato huo wa kumpata rais ndani ya CCM ufanywe na Mungu,” alisema.
Dk.
Magufuli alisema wale wanaosalimia kwa kutumia salamu na kauli mbiu ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Peoples Power, wampe ‘power’
aende Ikulu kuharakisha maendeleo ya watanzania.
“Nipeni wabunge na madiwani wa CCM nikafanye kazi, tutafanyakazi bila kinyongo, hatutawabagua, hapa ni kazi tu,” aliahidi.
Alisema
maendeleo hayana chama, kabila wala rangi, hivyo amepanga kufanya kazi
na makundi yote bila kubagua na kuomba kura kwa wananchi wote bila ya
kujali vyama vyao vya siasa.
“Hakuna
anayezaliwa kutoka tumboni mwa mama yake akiwa na kadi ya chama fulani,
bali wanavikuta, hivyo msidangaywe na vyama, kinachotakiwa ni
maendeleo,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu madai ya walimu nchini, alisema kada hiyo siyo wito bali ni
kazi, fedha na kuwafundisha wanafunzi kwenye shule walizopangiwa na
serikali.
Alisema baada ya kuingia Ikulu, kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuwalipa madeni wanaoyoidai serikali.
Magufuli aliwataka walimu kuwa wavumilivu na kuwaomba kumchagua kwa kura nyingi katika uchaguzi huo.
“Sitawaangusha,
nitamtanguliza Mungu na kila mmoja katika sala zake aniombee nisijeanza
kwa kiburi, kujiona, kusahau ahadi, niwe mtumishi wa watu, nikapendwe
kwa utumishi na siyo bora utumishi,” alisema.
Post a Comment