Kundi
la watu zaidi ya 100 wakiwa na silaha mbalimbali za jadi ikiwemo
mapanga, mawe na marungu wamevamia kituo kidogo cha polisi cha Mbingu,
kilichopo tarafa ya Mngeta wilayani Kilombero, kukipiga mawe na
kukichoma kwa moto, wakishinikiza kukabidhiwa ili wamuue mtuhumiwa
waliyemfikisha polisi muda mchache kabla, aliyekuwa akituhumiwa kumuua
mkewe kutokana na wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo lililothibitishwa na polisi, limetokea kituo kidogo cha
polisi cha Mbingu kilichopo umbali wa takribani kilometa 60 kutoka mji
mdogo wa Ifakara, ikiwa ni saa chache baada ya mtuhumiwa Bashiri Ernest
Kadugula kufikishwa kituoni hapo akikabiliwa na tuhuma za kumuua mkewe,
Veronica Chambula kwa kumkata kata kwa panga, baada ya kutokea tofauti
baina yao, na mke kuamua kukimbilia kwa wazazi wake, lakini mumewe
alidhani alikuwa amekwenda kwa mwanaume mwingine.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo amesema polisi
walifanikiwa kumtorosha mtuhumiwa Kaduguda aliyekuwa akitafutwa,
sambamba na baadhi ya silaha, kabla ya wananchi hao kukipiga mawe na
kukiteketeza kwa moto kituo hicho cha polisi na kusababisha pikipiki
tano zikiwemo mbili za askari polisi, PC Wilson na PC Isaya kuteketea,
sambamba na kuvunja mlango wa ofisi ya kijiji cha mpofu na kuchoma moto
nyaraka mbalimbali zilizokuwemo, na tayari watuhumiwa 11 wametiwa
mbaroni kuhusiana na tukio hilo.
Kufuatia tukio hilo, wananchi wa mkoa wa Morogoro wamelaani matukio
ya waanchi kuvamia vituo vya polisi na ofisi nyingine za serikali,
kuzichoma moto na hata kusababisha hasara mbalimbali.
Post a Comment