Madereva wa daladala mkoani Morogoro wamegoma kutoa huduma za usafirishaji wakishinikiza kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili sambamba na kuachiwa kwa wenzao wawili waliokamatwa siku takribani sita zilizopita kwa madai ya kutishia kumgonga askari wa usalama barabarani na mwingine kudaiwa  kusafirisha mafuta ya petroli kinyume na utaratibu.

Wakizungumza na ITV baadhi ya madereva wameeleza kusikitishwa na uonevu waliodai wenzao kufanyiwa na baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi kwa kubambikiwa makosa huku wakinyimwa dhamana au kufikishwa mahakamani, kukamatwa na maafisa wa mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu Sumatra kwa madai ya kuibia njia pale wanapoamua kusaidia huduma maeneo ya mbali ambayo hayajapangiwa njia rasmi na ubovu wa muda mrefu wa miundo mbinu.
 
Kufuatia mgomo huo, adha kubwa imewakumba wananchi wakiwemo wanafunzi na wakazi wengine, huku wengi wakishindwa kwenda makazini na kwenye shughuli zao hvyo kulalamikia mamlaka husika kushindwa kutatua changamoto hizo hadi kusababisha mgomo huo.
 
Akizungumza baada ya kikao cha dharura kilichoshirikisha uwakilishi wa madereva, jeshi la polisi, Sumatra na viongozi wa manispaa, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo amesema wamekubaliana madereva hao kusitisha mgomo na kurudi  barabarani, na kwamba wataimarisha ushirikiano miongoni mwao na kwa pamoja kutatua kero zilizolalamikiwa.

 

 

Post a Comment