CHAMA cha ACT-Wazalendo kimefuta mikutano yote ambayo aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alikuwa aifanye kuanzia kesho
kupitia jukwaa la chama hicho.
Sababu kubwa imeelezwa ni hofu juu ya usalama ya Dk Slaa ambaye
ameachana na siasa tangu chama chake kilipoamua kupokea wanachama wapya
kutoka CCM, wakiongozwa na Edward Lowassa ambaye ndani ya muda mfupi
amepewa heshima kubwa na hata kufanywa mgombea urais wa chama hicho,
nafasi aliyokuwa anaitaka ndani ya CCM, lakini hakupitishwa na vikao
muhimu vya chama hicho tawala hivyo kuamua kuhama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam
jana na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, Dk Slaa tayari
alishakubali kupanda jukwaa moja na chama hicho katika kampeni
zinazoendelea kwa lengo la kuendeleza vita dhidi ya ufisadi nchini.
“Tunamshukuru sana Dk Slaa kwa imani aliyo nayo juu ya chama chetu na
uamuzi wake wa kuikabidhi rasmi ACT-Wazalendo, mikoba yake ya vita
dhidi ya ufisadi nchini,” alisema Mwigamba.
Alisema Dk Slaa anaamini kwamba chama hicho cha ACT ndicho chama
pekee chenye uhalali na uwezo wa kupambana na ufisadi baada ya chama
chake cha zamani (Chadema) kuitelekeza vita hiyo.
Alisema mwanasiasa huyo ilikuwa ashiriki kikamilifu katika kampeni za
uchaguzi zinazoendelea kupitia jukwaa la ACT na alitakiwa aanze na
mkutano wa hadhara Iringa Oktoba 7, mwaka huu na baadaye angeendelea na
mikutano mingine katika majimbo mbalimbali na kuhitimisha kampeni hizo
katika Viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam.
Post a Comment