Mjumbe wa kamati ya kampeni ya chama cha  Mapinduzi, Christopher Ole Sendeka amelaani kitendo cha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kuruhusu vijana kusafisha barabara ya lami ili msafara wake upite akidai  kuwa  huo  ni  utumwa.

Ole Sendeka  alitoa  kauli  hiyo  jana  wakati  akiwa katika mkutano wa kumnadi mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan mjini Geita.

Juzi mjini Musoma na jana Jijini Mwanza walijitokeza vijana na kupiga deki barabara ili Lowassa apite, wakisema hawataki apate mafua.

Sendeka jana alikemea kitendo hicho katika mikutano kadhaa mkoani Geita akisema, “Lowassa anatumia umaskini wa vijana wetu kuwalipa fedha ili wamwage maji kwenye barabara ya lami kusafisha barabara msafara wake upite. Huo ni utumwa si utumwa?” aliuliza Sendeka na kujibiwa na wananchi kwa sauti, “Ni utumwa.”

“Namtaka Lowassa asitumie nafasi yake ya ugombea urais kudhalilisha utu wa vijana kwa sababu ya fedha zake, tena ambazo hakuzipata kihalali kuwalipa vijana wetu eti wakamsafishie barabara ya lami apite,” alisema.

Sendeka alisema kitendo hicho cha aibu kimeona matairi ya gari la Lowassa yana thamani kuliko utu wa vijana.

“Kama kweli hakufadhili mpango huo wa kulipa vijana wafanye hivyo kwa nini hakuwakataza alipoona wanamwaga maji ili msafara wake upite,” alihoji.

 

Post a Comment