Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello
amepasua ukweli wa kusuasua kwa klabu bingwa nchini humo Chelsea, ambayo
imeshindwa kuonyesha mwanzo mzuri msimu huu.
Capello ambaye aliachana na timu ya taifa ya Urusi Julai 14 mwaka
huu, amesema kuanza vibaya kwa klabu hiyo ya jijini London kumetokana na
mazoea ya meneja wao Jose Mourinho ambayo yamekua yakimgharimu mara kwa
mara.
Capello, amesema Mourinho hakuwandaa vyema wachezaji wake katika hali
ya kupambana wakati wote na badala yake aliamini msimu huu, huenda
ungekua na sura sawa na ule uliopita ambao ulimalizika kwa Chelsea
kutwaa ubingwa.
Amesema anashangazwa na baadhi ya watu kuwanyooshea vidole wachezaji
wa The Blues, kwa kuwatuhumu wamekua hawajitumi, lakini kwake analiona
tatizo lipo kwa mkuu wa kikosi hicho.
Capello, amekumbushia hali kama hiyo iliwahi kutokea, wakati Mourinho
akiwa na kikosi cha klabu ya Real Madrid, ambapo baada ya kutwaa
ubingwa wa nchini Hispania msimu wa 2011–12, alibweteka na msimu
uliofuata hakufanya vyema na ndio ukawa mwisho wake huko Estadio
Stantiago Bernabeu.
Kutokana na maelezi hayo, Capello ametoa angalizo kwa mashabiki
pamoja na viongozi wa klabu ya Chelsea, kuwa na mtazamo chanya kwa Jose
Mourinho, kwani anachokifanya kwa sasa hakistahili kuendelezwa zaidi ya
kubadili mbinu za upambanaji.
Mpaka sasa Chelsea wameshapoteza michezo minne ya ligi ya nchini
England, wameshinda miwili na kutoka sare mara mbili, hali ambayo
imeifanya klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London, kusalia katika
nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi kwa kumiliki point nane.
Post a Comment