Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar,
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad amehoji sababu za
chama tawala, CCM kuhofia CUF kuongoza visiwa hivyo.
Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 ambao matokeo yake yalifutwa, pia amesema endapo CCM itasitisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika siku 36 zijazo, CUF watakuwa tayari kufanya mazungumzo lakini si kwa wakati huu ambao maandalizi ya kupiga kura yanaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katibu
huyo mkuu wa CUF aliitoa hofu CCM kuwa chama chake hakina ajenda ya
kulipiza kisasi.
Matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar,
wawakilishi na madiwani yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
(ZEC), Jecha Salum Jecha siku ambayo chombo hicho kilitakiwa kumtangaza
mshindi, na mwezi uliopita alitangaza Machi 20 kuwa siku ya uchaguzi wa
marudio visiwani humo.
Wakati CUF ikipinga vikali kufutwa
matokeo na kutangaza tarehe mpya, Serikali imesema kuna nafasi ya
kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna muda
mrefu wa kufanya hivyo.
Jecha alitangaza uamuzi huo wakati
tayari matokeo ya urais ya majimbo 31 yalishatangazwa, na ya majimbo
tisa yaliyosalia yalishahakikiwa, huku washindi wa viti vya uwakilishi
na udiwani wakiwa wametangazwa na kupewa vyeti vya ushindi.
“Sijui kwa nini CCM wanaogopa sisi tukiongoza?” alihoji Maalim Seif
kwenye mkutano huo na waandishi akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais
wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
“Wana wasiwasi gani, kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.
Katika
mkutano huo, Maalim Seif mbaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho
alisema kama CCM ina wasiwasi na idadi ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), haina budi
kuondoa shaka kwa kuwa idadi kwa pande zote inakaribiana.
“Hawa wanahisi hawatapata uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya wawakilishi?” alihoji.
Kuna Vitisho Zanzibar
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema kumekuwapo
vitendo vya wananchi kupigwa na vikundi vya watu wasiojulikana.
Alidai
wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake wameamrishwa kupeleka
vitambulisho vyao vya kazi na vya kura serikalini ili vikahakikiwe.
“Hii
si mara ya kwanza wafanyakazi wa Serikali kutakiwa kupeleka
vitambulisho, sisi tunajua kuwa wanataka wawatishe kuwa watajua nani
kapiga kura na nani hajapiga,” alisema na kusisitiza:
“Hii ni kama
kitisho cha kuwalazimisha wakapige kura, zaidi hasa hizo ni dhuluma
ambazo wananchi wanafanyiwa.”
Kadhalika Maalim
Seif alizungumzia uwapo wa watu wanaovaa soksi usoni na kuwashambulia
raia, akisema Serikali haijachukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.
Alisema
watu hao ambao wamepachikwa jina la mazombi, wamevamia maeneo kadhaa
kama Baraza la CUF, Jang’ombe na yaleambayo yana wafuasi wa chama hicho
kikuu cha upinzani visiwani humo.
“Wanawapiga watu, wanawajeruhi
na wanaiba mali, lakini inashangaza sana mambo haya na si Serikali wala
polisi iliyochukua hatua,” alisema.
Maalim Seif alisema
amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu matukio
hayo ya uharamia wanaofanyiwa wananchi, lakini hakuna hatua
zinazochukuliwa.
Alisema CCM wanatafuta sababu ili machafuko zaidi yatokee visiwani humo wapate kisingizio.
Aliwataka
wafuasi wa CUF kuvumilia hali hiyo ili nchi isiingie kwenye machafuko
kama yaliyotokea mwaka 2000, wakati watu zaidi ya 20 waliuawa na wengine
kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya ambako waliishi kama
wakimbizi.
Lowassa Azungumza
Kwa upande wake, Lowassa aliwataka viongozi wa ngazi za juu wachukue hatua kumaliza mgogoro wa Zanzibar.
“Hili tulichukulie kwa umakini sana. Viongozi wafanye vikao vya maridhiano, tunaipenda sana amani tuliyonayo,” alisema.
Lowassa alisema anashangazwa na jinsi CCM wanavyoshindwa kuheshimu makubaliano ya SUK na kukataa kukubali matokeo.
ZEC yagoma kuondoa picha ya Maalim
Wakati
huohuo, habari zinaarifu kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar( ZEC)
imegoma kuondoa picha za wagombea Urais,Udiwani na Uwakilishi
kutoka vyama vilivyotangaza kutoshiriki uchaguzi wa
marudio,ikiwemo jina na picha Maalim Seif Sharif Hamad.
Hilo
lilifahamika jana mjini Unguja baada ya kigogo mmoja wa ZEC
ambaye hakuwa tayari kutaja jina kusema kuwa sheria hazimruhusu
mgombea yeyote kujitoa mwenyewe kwa utashi wake binafsi.
Kiongozi huyo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984,mgombea hawezi kujiondoa kwa utashi wake baada ya Tume kukamilisha kazi ya uteuzi ambayo ilifanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka jana.
"Ieleweke
kwamba mgombea urais anaweza kujiondoa katika kinyang'anyiro kwa
kuwasilisha taarifa za maandishi yeye mwenyewe ofisi za ZEC
kabla ya saa 10 jioni ya siku ya uteuzi." Alisema ofisa huyo akinukuu kifungu cha katiba.
Alisema
uteuzi wa mgombea mwingine unaweza kufanyika ndani ya siku 21
kama mgombea hatafariki dunia,lakini hakuna ruhusa ya kujitoa
kabla ya kukamilika kwa uchaguzi.
Alisema
ZEC tayari imeviandikia vyama kuvitaka vithibitishe iwapo
wagombea wao wangali hai au kuna waliofariki dunia, na si kutaka
kufahamu kama watashiriki uchaguzi wa marudio au la.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF anena
Mkurugenzi
wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe amesema ZEC
inasuka mkakati wa siri wa kutaka kuzitumia picha na taarifa
za wagombea wao kwa lengo la kuidanganya dunia na jumuiya za
kimataifa kwamba CUF walishiriki uchaguzi huo.
Shehe
amesema CUF kilitangaza mapema kabisa kutoshiriki uchaguzi wa
marudio,hivyo dunia nzima inaelewa kabisa kwamba CUF haishiriki
uchaguzi huo na kitendo cha kuendelea kuchapisha picha na
taarifa za wagombea wao katika karatasi za wapiga kura si
sahihi.
Post a Comment