Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini
(WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi.
Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha
mafuta bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu
kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni
jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu
wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za
kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda
popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi
hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya
TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika
kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika
basi watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow
meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara
moja.
Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara
kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na
kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa
Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh.
bilioni 12.96/- za sasa).
Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka
bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya
kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx
Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia
bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka
bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo
litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili
kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia
wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
Post a Comment