Shirika la umeme nchini Tanesco limeokoa shilingi bilioni 2.7 zilizokuwa zinapotea kutokana na ubovu wa miundombinu pamoja na tatizo la umeme kukatikakatika hovyo hali iliyokuwa ikilikosesha shirika hilo mapato.

Uokoaji wa kiasi hicho cha fedha umetokana na mradi ulioanzishwa na serikali ya Japan kwa kushirikiana na Tanesco wa kutoa utaalamu wa mafunzo kwa mafundi wa Tanesco ya namna ya kutumia teknolojia ya kisasa na kuboresha miundombinu ya usambazaji na usafirishaji umeme hali iliyosaidia kuepuka ukatikaji wa umeme mara kwa mara.
 
Kaimu mkurugenzi wa Tanesco Bw Decklan Mhaiki akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufungaji wa mradi huo awamu ya kwanza amesema kwa sasa hali ya uzalishaji wa umeme imeimarika baada kiwango cha maji katika mabwawa kuongezeka pamoja na uzalishaji wa gesi.
 
Kwa upande wake mwakilishi wa JICA Bw Toshio Nagase amesema katika mradi huo wameweza kuwapatia mafunzo kwa vitendo mafundi 1,400 wa Tanesco na kwamba suala la kuendelea na mradi huo awamu ya pili linawezekana baada ya serikali ya Tanzania kuomba.
 

Post a Comment