Siku mbili baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema Wilaya ya Temeke inaongoza mkoani Dar es Salaam kwa kuwa na wagonjwa sita wa kipindupindu, Mkuu wa wilaya hiyo (DC), Sophia Mjema amesema hadi jana hakukuwa na mgonjwa hata mmoja.

Baada ya DC huyo kukanusha, jana wizara hiyo ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na ugonjwa huo.

Kipindupindu ni moja ya vigezo vinne vilivyowekwa na Rais John Magufuli kupima utendaji kazi wa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kabla ya kufanya uteuzi mpya.

Jumatatu iliyopita akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Waziri Ummy alitoa takwimu za ugonjwa huo na kuitaja Temeke kuwa kinara lakini juzi, Mjema alisema kulikuwa na wagonjwa ambao hawakuwa wamethibitika kama wanaugua kipindupindu.

Jana, Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema juzi kulikuwa na mgonjwa mmoja wa kipindupindu lakini aliruhusiwa baada ya kupona.

“Kwa hiyo leo (jana) Manispaa ya Temeke haina hata mgonjwa mmoja na kambi ni nyeupe haina mtu,” alisema.

Alisema manispaa hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kanuni za afya ili kujikinga na ugonjwa huo baada ya kufanikiwa kuutokomeza.

“Hatutapumzika tutaendelea kuwakumbusha wananchi kutunza mazingira yao kuwa safi kwa sababu kipindupindu ni hatari,” alisema.

Wakati ofisa hiyo akisema hayo, Waziri Ummy alitoa taarifa akisema Mkoa wa Dar es Salaam kwa siku 10 zilizopita kuanzia Februari 7 hadi 16 kulikuwa na wagonjwa 16; Temeke 12 na Ilala wanne.

Alisema wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kusimamia huduma za afya kwa jamii, hivyo wagonjwa hao walikidhi vigezo vya ainisho sanifu na kupata matibabu katika kambi ya kipindupindu kwa wagonjwa wa Temeke na Hospitali ya Amana kwa wagonjwa wa Ilala hivyo kulazimu kutolewa taarifa kwa mujibu wa mwongozo.

Post a Comment