NAIBU
Spika Dk. Tulia Mwansasu, amepata ajali mkoani Mbeya alikokwenda kwa
ajili ya mapumziko. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Zainab
Mbussi, Dk. Tulia alipata ajali hiyo jana wakati akitokea Mbeya mjini
akielekea Kyela.
Mkuu wa wilaya alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Shule ya Sekondari ya Kipoke iliyoko wilayani humo.
Alisema
maelezo ya askari wa usalama barabarani, yanaeleza kuwa chanzo cha
ajali hiyo ni gari dogo lililoelezwa kuwa liliibeba familia ya mtu
aliyetajwa kwa jina moja la Chacha, lililokuwa likitokea Kyela kwenda
Mbeya, lilipojaribu kulipita lori na kukutana na gari la Naibu Spika.
Zainab
alisema Dk. Tulia, mdogo wake pamoja na mlinzi wake waliokuwa kwenye
gari lake wako salama ingawa gari hilo limeharibika vibaya sehemu za
mbele.
Aidha,
alisema baadhi ya abiria waliokuwa kwenye gari la Chacha wakiwemo
wanawe wawili walipata majeraha na walipelekwa katika hospitali ya
Mission Igogo, Kiwira.
Awali
mapema jana, Dk. Tulia, alitoa msaada wa sh. milioni tano, ili
kulifanyia ukarabati bweni la Mapinduzi, ambalo alikuwa analala wakati
anasoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza, iliyopo jijini Mbeya.
Dk.
Tulia ambaye alisoma shuleni hapo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha
nne, mwaka 1991 hadi 1994, pia alitoa msaada wa magunia mawili ya mchele
kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi.
Akizungumza
na walimu na wanafunzi, Dk.Tulia alisema ametajiwa changamoto nyingi,
zinazoikabili shule hiyo na kuwa amzichukua na kuahidi kutafuta wadau
atakaoshirikiana nao ili waweze kusaidia kuzitatua.
Dk.
Tulia alisema ameguswa na uchakavu wa mabweni, ambapo alipata fursa ya
kuonyeshwa yakiwemo mawili aliyokuwa analala akiwa shuleni hapo, ambayo
ni Kibo linaloendelea kutumika hadi sasa na lile la Mapinduzi ambalo kwa
sasa halitumiki.
“Kwenye
bweni nililokuwa nikikaa nimepita mwenyewe. Naahidi kushughulika na
lile bweni la Mapinduzi ndilo lililo kwenye hali mbaya zaidi kiasi cha
kushindwa kuendelea kutumika,” alisema Dk.Tulia.
Dk.Tulia
alitoa magunia mawili ya mchele, kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi
shuleni hapo na aliwachekesha wanafunzi pale aliposema katika mambo
ambayo hayajabadirika shuleni hapo ni ratiba ya kula wali mara mbili kwa
wiki.
“Kwa
sababu mimi dada yao nimewatembelea leo, na waswahili wanao msemo
‘mgeni njoo mwenyeji apone’, basi mimi nitawaletea magunia mawili ya
mchele ili angalau kwa hizi wiki wanafunzi wawe wananikumbuka,” alisema Dk.Tulia.
Naye,
mbunge wa Songwe, Philip Mulugo, alimuunga mkono Dk.Tulia kwa kuchangia
sh. milioni moja, kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa bweni hilo la
Mapinduzi.
Viongozi
mbalimbali wa Chama na serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya, Munasa Nyerembe, walikuwepo katika ziara hiyo na Naibu Spika
kutembelea shule hiyo ambayo hivi sasa inachukua wanafunzi wa kidato cha
tano na sita tu.
SOURCE: MPEKUZI
Post a Comment