BASATA limetoa makucha yake. Hii ni taarifa yake rasmi iliyotoka Ijumaa hii:
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limeufungia rasmi wimbo wa ‘Shika Adabu Yako’ ulioimbwa na Msanii Nay wa
Mitego kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili, kashfa, uchochezi,
kudhalilisha watu na kuhatarisha amani na utengamano miongoni mwa
wasanii na jamii kwa ujumla.
Sambamba na kuufungia wimbo huo, BASATA
litampa karipio kali Msanii huyo na kumwagiza kuacha mara moja
kujihusisha kwa namna yoyote na tabia ya kuutangaza wimbo au kuusemea
katika vyombo vya habari vinginevyo hatua kali zaidi na za kisheria
zitachukuliwa.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu
cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza
limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia mienendo ya mtu yeyote
anayehusika na kazi za Sanaa na kuhakikisha linalinda maadili ya kitaifa
miongoni mwa Wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya
Sanaa.
Aidha, kifungu cha 4 (2) cha sheria hii
kinalipa Baraza nguvu ya kisheria kufanya jambo lolote lile kuliwezesha
kufanya majukumu yake kwa faida na ustawi wataifa.
Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa
likipokea simu za maswali na malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa
habari na wadau wa Sanaa ambao kwa njia moja ama nyingine wameguswa na
kuchukizwa na kazi hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali
inawafanya watu makini kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma
ya Sanaa kwa ujumla.
BASATA mara kadhaa limekuwa likikemea na
kuchukua hatua kadhaa dhidi ya tabia hii chafu ambayo ilianza
kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana wa 2015.
Kukemea huku ni kwa msingi mmoja kwamba asili ya tasnia hii ya Sanaa ni
kuelimisha jamii, kukosoa pale kunapokuwa na tatizo, kuburudisha na
kujenga jamii yenye staha, umoja wa kitaifa, mshikamano na amani.
Ni wazi wasanii wengi wanafanya kazi zao
vizuri, kwa kubuni kazi zenye ubora, zenye kujenga jamii na zaidi
zinazoburudisha rika zote kiasi cha kuzifanya zililetee heshima taifa.
Kati ya hawa wengi, kuna wachache ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa
na kwa kiasi kikubwa wanaonesha wazi kutokuwa na nia njema.
Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia
hawa ‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa na
wasanii genge la wahuni, wasio na staha, wa kudharaulika na waliojipanga
kuibomoa jamii na kuharibu amani na utulivu uliopo nchini.
BASATA linapenda kueleza yafuatayo:
1. Vyombo
vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa
kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii
kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA lilishaziandikia radio zote
kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za Sanaa lakini inashangaza
baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia nyimbo hizo
chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na baadaye kurudi
BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata kidogo.
2. Serikali
ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga
kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii wote nchini kupitia
kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata hivyo, uwepo wa
Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii, nafasi yao
katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za kuipa msukumo
sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza kuoneasha kuwa
mawakala wa uharibifu wa jamii.
3. BASATA
linawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za
Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao watazipokeaje?
Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha, Waelewe kwamba
Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata kidogo. Ikitokea
wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa itakuwa uwanja wa
vita. Hili halikubaliki.
4. Tunafahamu
kuna wasanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta ‘umaarufu
uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumziwa sana.
Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna hiyo
unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora na
zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
Post a Comment