Dr.
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria amewataka Watanzania
wanaoulizia hatima ya mchakato wa katiba mpya kutambua kuwa suala hilo
si sehemu ya vipaumbele vya Dk. John Magufuli.
Mwakyembe
amesema hayo jana usiku katika mahojiano maalum aliyofanya na Marin
Hassan, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), juu ya
utendaji wa wizara yake katika siku 100 za serikali ya awamu ya tano.
Waziri
huyo alisema kuwa katiba mpya haina umuhimu mkubwa katika maisha ya
kila siku ya watu na wala sio kipaumbele cha rais Magufuli kwani ni
kiporo tu alichoachiwa na serikali ya awamu ya nne na atakifanyia kazi
wakati atakapoona inafaa.
“Watu
wanadhani katiba mpya ndiyo kila kitu, wanaona katiba ni muhimu kuliko
kulipia watoto waende shule, wanafikiri katiba mpya ikishapitishwa tu
basi kesho yake wataletewa mkate na chai kitandani jambo ambalo sio
kweli,” amesema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa: “Kwa
sasa rais bado anafanyia kazi vipaumbele vyake kwanza ikiwemo kusimamia
elimu bure, kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya serikali na kusimamia
uwajibikaji wa watumishi wa umma na hivyo kelele za katiba mpya hazina
msingi.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alisema Watanzania ambao bado wana
ndoto kuwa mchakato wa katiba mpya unaweza kuanzia katika hatua ya
kujadiliwa kwa rasimu ya katiba ya Jaji Joseph Warioba kuachana na wazo
hilo kwani limepitwa na wakati.
Alisisitiza
kuwa katiba iliyopendekezwa na kupitishwa na wajumbe wengi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ni halali kwani ilipatikana kwa mujibu wa sheria na
taratibu licha ya kususiwa na wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa
unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha
Wananchi (CUF), National League for Demokracy (NLD) na NCCR Mageuzi.
“Rais
alishasema alipohutubia bunge, kwamba kuna kiporo nimeachiwa, sasa mimi
nashangaa hawa watu! tena wengine wana shahada za sheria, wanaongea
nini? Hatua ya rasimu ya Warioba ilishapitwa na wakati na tayari tunayo
katiba pendekezwa,” aling’aka.
Mwakyembe
alihitimisha kwamba utakapofika wakati wa kulifanyia kazi suala la
katiba mpya, serikali ya awamu ya tano itaendelea na hatua ya kura ya
maoni ya katiba pendekezwa na sio vinginevyo.
Post a Comment