Tanzania imedhihirisha kuwa ni tajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi asilia baada ya kugundulika kwa gesi nyingine katika bonde la mto Ruvu yenye ukubwa wa ujazo wa futi trilioni 2.17.
Ugunduzi huo wa gesi asilia umefanywa na Kampuni ya Dodsal
Hydrocarbons and Power Tanzania Limited ambayo imekuwa inafanya shughuli
za utafutaji wa gesi na mafuta katika Mkoa wa Pwani.
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Pilavullathil Surendran alisema jana
katika mkutano wa wawekezaji wa gesi na mafuta ulioandaliwa na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, thamani ya gesi
iliyoko katika eneo hilo inafikia Dola za Marekani bilioni sita sawa na
Sh trilioni 12.
Ugunduzi huo mpya unafanya hadi sasa Tanzania kuwa na amana ya gesi yenye ukubwa wa futi za ujazo trilioni 57.27.
Kwa upande wake, Profesa Muhongo alithibitisha kugundulika kwa gesi
hiyo tangu Julai mwaka jana, lakini akaeleza kuwa Serikali imechelewa
kutangaza ugunduzi huo kama inavyoagizwa na Sheria ya Mafuta ya Mwaka
2015 kutokana na shughuli za uchaguzi.
“Sheria mpya inatutaka kabla ya waziri mwenye dhamana ya gesi
kutangaza ugunduzi mpya wa gesi na mafuta ni lazima athibitishiwe na
mamlaka ya udhibiti wa bidhaa za Petroli na Gesi (PURA).
“Wizara yangu itawasiliana na mwanasheria mkuu wa serikali ili kupata
ushauri wa kisheria kuhusu jambo hilo na bahati nzuri tayari PURA
imeshaanza kushughulikia jambo hilo na naamini kuwa nitatangaza ugunduzi
huo mpya hivi karibuni,” alifafanua Profesa Muhongo.
Licha ya ugunduzi huo mpya tayari gesi imegundulika katika maeneo ya
kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi na eneo la Mnazi Bay huko Mtwara na
katika Wilaya ya Mkuranga, Pwani pia kumegundulika kiasi kikubwa cha
gesi.
Post a Comment