Serikali
imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa
katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa katika sekta hiyo
wakitumia vyeti bandia .
Aidha,
imewataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe
kabla ya kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na
utumishi wa umma yanayokuja nchini.
Kauli
hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako wakati wa majumuisho ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya mabadiliko makubwa katika
Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha kuwa Elimu inayotolewa katika
shule, vyuo na taasisi mbalimbali inazalisha wahitimu wenye sifa na
ubora kwa maslahi ya Taifa .
Amesema
katika kulitimiza hilo Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu
na kisheria watendaji wote walioshiriki na wale wanaoendelea kushiriki
kwa namna moja au nyingine kukwamisha maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni
pamoja na wale waliohusika katika udahili wa wanafunzi wasio na sifa
katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.
"Serikali
ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati kabisa kuboresha kiwango cha
elimu yetu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, naomba
niwahakikishie kwamba pale panapohitajika kufanyika mabadiliko
tutayafanya bila woga" Amesisitiza.
Amesema
katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini,
serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa elimu ambao umekuwa
ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko hayo yatafanyika kwa
kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.
"
Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa elimu tumekubali
kwamba tuna changamoto, katika changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa
kuanzia hivyo tunapochukua hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono" Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Prof.Ndalichako
Amesema lengo la Serikali kupitia Wizara yake ni kuhakikisha sekta ya
elimu inaboreshwa hapa nchini kwa kuendelea kutoa wahitimu bora
wanaokidhi vigezo na viwango katika soko la ajira.
Amesisitiza
kuwa mkakati wa Serikali ni kuanza kuwafuatilia wahitimu wote wasio na
viwango ambao wako katika maeneo mbalimbali ya ajira huku akisisitiza
kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na kiwanda kinahitaji malighafi nzuri
ili kitoe bidhaa bora.
Ameeleza
kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuvikagua vyuo vyote vinavyotoa
elimu ya juu kuona kama vinakidhi sifa na vigezo vya kiutendaji ili
hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote wanaowadanganya wananchi
na kuwapotezea muda vijana wanaowadahili bila kuzingatia sifa.
"Wizara
yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta hii muhimu,
tulichofanya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo
vingine"
Kuhusu
ujenzi wa maabara amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi
Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwa shule zote 1536
ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya maabara kote nchini.
Katika
hatua nyingine amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017
itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii kote nchini ili
majengo ya vyuo hivyo yaweze kutumika kuanzishia vyuo vya Ufundi Stadi
VETA katika wilaya na mikoa ili kuwapatia stadi za kazi vijana waweze
kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.
Kwa
upande wao baadhi ya Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia wakati wa
Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo wameiomba Serikali kuweka mkazo katika
usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili shule, Taasisi na vyuo vya
Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya Taifa.
Aidha,
wameiomba Serikali kupitia Bajeti hiyo itenge fedha za kutosha kwa
ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa shule, kuboresha maslahi na
kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha Mamlaka za Udhibiti wa
Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Post a Comment