Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, jana alikuwa katika wakati mgumu baada
ya kuzomewa na wananchi wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mama na
Mtoto mjini Arusha.
Tukio
hilo lilitokea wakati kiongozi huyo alipozungumzia mradi wa ujenzi wa
hospitali hiyo na kudaiwa kupotosha ukweli wa mradi huo.
Katika
maelezo yake, Gambo alisema eneo la hospitali hiyo lilitolewa na
familia ya Nyaga Mawalla, jambo ambalo wananchi walilipinga
wakishirikiana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).
Hospitali
hiyo itakayogharimu Sh bilioni tisa, inajengwa kwa wafadhili ambao ni
Taasisi ya Maternity Afrika, Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na
Mbunge Lema.
Kabla
mkuu huyo wa mkoa hajazomewa, alipewa nafasi ya kuzungumza na ndipo
alipoeleza jinsi familia ya Mawalla ilivyotoa eneo hilo.
Wakati
akitoa kauli hiyo, Lema ambaye alikuwapo mahali hapo, alisimama na
kupaza sauti akisema, “mkuu wa mkoa anapotosha ukweli wa mradi huu”.
Hatua
hiyo ya Lema kulalamika kwa sauti, iliwafanya wananchi nao kumzoea
Gambo huku baadhi yao wakimtuhumu kuingiza siasa katika shughuli za
maendeleo.
Kutokana
na zomeazomea hiyo, polisi waliokuwapo mahali hapo wakiwa na silaha
za moto na mabomu ya machozi, walilazimika kusogea eneo la meza kuu huku
wengine wakimzunguka Gambo aliyekuwa akiendelea kubishana na Lema
kuhusu ukweli wa mradi wa hospitali hiyo.
“Huyoo,
acha kupotosha ukweli wewee, usilete siasa kwenye maendeleo, huyooooo,”
zilisikika sauti za wananchi kutoka upande wa pili wa meza kuu huku
Lema naye akisikika akihoji kwa nini mkuu huyo wa mkoa alikuwa akisema
uongo.
Katika
hotuba yake ambayo pia ilikatishwa baada ya kutokea kelele hizo, Gambo
aliishukuru familia ya marehemu Mawalla kwa kile alichosema ilitoa eneo
hilo na kuwatafuta wafadhili wa kujenga hospitali hiyo.
“Hili wazo lilikuwa ni la familia ya Mawalla kwa sababu ardhi ni mali yao na walikuwa na maono ya kujenga hospitali hii.
“Kwa hiyo, Serikali itakuwa pamoja nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnafanikiwa,” alisema Gambo huku akizomewa na wananchi.
Wafadhili
kutoka Ulaya waliokuwa kwenye uzinduzi huo, walijikusanya makundi na
kumkumbatia Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maternity Afrika, Andrew Brown,
wakimpa pole kwa kile kilichotokea.
Hata
hivyo, baadhi ya wafadhili hao walianza kulia wakionyesha ni kwa kiasi
gani hawakuridhishwa na mvutano kati ya mkuu wa mkoa, mbunge na
wananchi.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya uzinduzi huo, Lema alisema mkuu huyo wa
mkoa alifanya makosa kuupotosha umma kuhusu mradi huo.
“Mkuu wa mkoa alitakiwa kufika saa 4.00 asubuhi lakini hakuonekana kwa madai kwamba asingeweza kuja kama mimi nipo.
“Ilipofika
saa saba kasoro bila kumuona, nikampigia simu Katibu Mkuu Kiongozi,
John Kijazi kumweleza suala hili, naye akampigia simu Katibu Mkuu
Tamisemi.
“Inavyoonekana Tamisemi walimpigia simu mkuu wa mkoa ndipo akaamua kuja akiwa amechelewa.
“Kwa hiyo, kilichofanyika hapa kinaonyesha aina ya viongozi walioaminiwa na Rais John Magufuli wamsaidie kuongoza nchi.
“Wafadhili walimualika kuipa heshima Serikali, lakini hakuonekana hadi alipopewa maagizo.
“Kwa faida ya wasiofahamu ni kwamba mimi kupitia ArDF ndiyo tuliotafuta ardhi kwa marehemu Nyanga Mawalla.
“Kibaya zaidi, alipofika hapa akaagiza ratiba ibadilishwe mimi nisizungumze kwa sababu anazozijua yeye.
“Ushahidi
wa ratiba hiyo ni kwamba, ilipangwa azungumze mtendaji mkuu wa
Maternity Afrika, kisha mkurugenzi wa ArDF, baadaye mimi mbunge pamoja
na Mawalla kutoa historia ya mradi na mwisho mkuu wa mkoa.
“Lakini, ratiba hiyo haikufuatwa na badala yake alifanya anavyojua yeye mradi tu nisizungumze.
“Sasa,
hivi unawezaje kuwalazimisha Maternity Afrika wasinilete mimi wakati
kwenye mkataba wa hili eneo mimi na ArDF ndiyo wasimamizi wa mradi?”
alihoji Lema.
Mwenyekiti wa ArDF, Elifuraha Mtoi, alisema Taasisi ya ArDF kwa kushirikiana na Lema ndiyo waliofanikisha mradi huo.
“Hizi
ni jitihada binafsi za ArDF kwa sababu baada ya kupata wafadhili,
tuliwaunganisha na Mawalla Trust ambao ndiyo wamiliki wa maeneo haya.
“Kwa hiyo, kilichofanywa na mkuu wa mkoa kimetufedhehesha mbele ya wafadhili,” alisema Mtoi.
Awali,
Mtendaji Mkuu wa Maternity Afrika (Brown), alisema fedha za ujenzi wa
hospitali hiyo zitatokana na michango mbalimbali ya wafadhili na sadaka
kutoka makanisani.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa ambaye pia ni mmoja wa
waaanzilishi wa Taasisi ya ArDF, alimtangaza Gambo kama adui wa
maendeleo mkoani Arusha.
Post a Comment