SeeBait

Mtoto Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa ni mhalifu, maarufu Panya Road, amezinduka akiwa chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) katika Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.

Isack ni miongoni mwa vijana watano waliopigwa na wananchi wenye hasira kwa madai ya kuiba mali zao hali iliyosabisha apoteze fahamu na kudhaniwa amefariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Gilles Muroto, alisema baada ya polisi kupigiwa simu na raia wema kuwa kuna vijana watatu wamefariki dunia, walikwenda eneo la tukio na kuwakuta wakiwa na hali mbaya.

“Mmoja wao anayeitwa Kelvin Nyambocha (14) alifariki dunia baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi.
 
“Kabla ya kufariki, Kelvin alifuatana na wenzake kwa lengo la kwenda kuangalia tamasha la kuibua vipaji vya muziki wa singeli lililoandaliwa na Radio Clouds Fm lililofanyika Mbagala Zakhem,” alisema Kamishna Muroto.

Alisema wakati wanarudi nyumbani, kundi la vijana hao wanaojiita Panya Road waliokuwa na silaha za jadi (mapanga), waliwavamia watembea kwa miguu na kuwaibia mali zao na ndipo wananchi walipofanikiwa kuwakamata watano. 
Alisema Isack alipigwa hadi akazimia kiasi ambacho walijua amefariki dunia na ndipo alipopelekwa chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo na kuwekewa namba tayari kwa kuingizwa kwenye jokofu.

“Wakati amewekwa chini kwa ajili ya kuingizwa kwenye jokofu, alizinduka kwa kupumua na kuonekana bado yupo hai, hali iliyosababisha kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU),” alisema Kamishna Muroto.

Alisema baada ya kupata fahamu na afya yake kutengemaa, alihojiwa na Jeshi la Polisi, akawataja wenzake 10 waliokuwa kikundi kimoja. Vijana hao ni Menso Somba (16), Adam Jumanne (16), Bakari Amir (14), Ally Said (17), Abdillah Yusuf (16), Brown Mathias (15), Jafari Salum (13), Hamisi Mwanda (16), Siraji Hamisi (16) na Jeremia Gaudence (13).

Wakati vijana hao wakipewa mapanga yao mbele ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Temeke huku wazazi wao wakishuhudia, walianza kuyagombea wengine wakidai kuwa yao yamebadilishwa na kupewa wenzao.

Kamishna Muroto alisema kikundi hicho kina bendera inayoonyesha michoro mbalimbali ikiwamo askari mwenye silaha anakimbia huku anatiririka damu, mtu ameanguka chini akiwa amekatwa mkono, nyumba na vijana wawili wakiwa wameshika panga.

Alisema kundi hilo la vijana ambalo linazunguka maeneo mbalimbali, limekuwa likijiita ‘Taifa Jipya’.

Kamishna Muroto alisema kijana mwingine, Faraji Suleiman (19) ambaye pia hali yake ni mbaya, amelazwa Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Kamanda Muroto alisema vijana wawili aliowataja kuwa Hamisi Mponda (18) na Abdallah Omari (15) walitibiwa hospitali ya Temeke na kuruhusiwa.

Alisema jeshi hilo kupitia Sheria ya Watoto ya mwaka 2009 kifungu 7-9, linakusudia kuwafikisha mahakamani wazazi wa watoto 16 ambao walitajwa na kuthibitisha kufanya uhalifu huo, kwa kushindwa kuwaangalia watoto wao.

Kamishna Muroto alisema wazazi wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anakuwa chini ya uangalizi ambao hauwezi kumsababishia madhara ya kimwili na kisaikolojia.

“Hii ina maana kila mzazi ahakikishe mtoto wake ana ulinzi, yuko salama muda wote dhidi ya udhalilishaji na hatari zote ili watoto hawa wakue vizuri,” alisema Kamishna Muroto.

Alisema jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anakuwa kwenye malezi bora na si kumwacha akilelewa na walimwengu.

“Mzazi atakayeshindwa kumsimamia vyema mtoto wake na kukiuka sheria ya mtoto ya mwaka 2009 katika kifungu cha 14, atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atafungwa miezi 6 au kulipa faini ya Sh milioni 5,” alisema Kamanda Muroto.

Alisema kutokana na mazingira waliyokutwa watoto hao, wazazi wao wanatuhumiwa kwa kukiuka sheria hiyo ya watoto.

Akisimulia mkasa huo, Isack Ernest alisema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na hajawahi kufanya vitendo vya kihalifu.

Alisema wakati yupo kwao, wenzake walimfuata na kumwambia waende kwenye tamasha la singeli Mbagala.
 
“Tulienda na baada ya kumaliza tamasha, wenzangu wakasema twende tukale (walimaanisha wakapore), mimi nikajibu sina pesa, ndipo waliposema wakienda kula hawatanigawia kwa kuwa aliyekula kala, ndipo walipokwenda kuvamia watembea kwa miguu na kuiba.

“Wakati nikiwa ng’ambo ya pili, nikasikia sauti ya watu wanasema mwizi mwizi, mwizi,” alisema Isack.
 
Alisema baada ya kupigiwa kelele za wezi, walikimbia na kumfuata alipo ndipo kipigo kilipomwangukia yeye hadi kupoteza fahamu.

“Nilikuja kushtuka nipo ICU, huku nikiwa sijui niko wapi, nimekoma kujihusisha na makundi kwa sababu sijawahi kuiba katika maisha yangu,” alisema Isack.

Baba mzazi wa kijana huyo, Ernest Chalo, alisema mtoto wake alimuaga anakwenda kuangalia mpira Mbagala Oktoba 15, mwaka huu.

Alisema wakati yeye anafuatilia mchezo wa timu ya Simba na Kagera Sugar, alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akimpa taarifa ya kuwa mtoto wake amefariki dunia.
“Kiukweli nilichanganyikiwa kwa sababu nimetoka kumzika mke wangu wiki moja iliyopita, tena napokea taarifa ya mtoto kufariki, nilitoka mpaka kwa mwenyekiti wangu wa mtaa na kumpa taarifa, nikachukua usafiri wa pikipiki kwenda Hospitali ya Temeke,” alisema Chalo.

Alisema alipofika hospitalini hapo, aliambiwa mtoto wake yupo chumba cha kuhifadhia maiti, lakini alipoletewa mwili kuutambua haukuwa wa mtoto wake, ndipo akatokea msamaria mwema akamwambia mtoto wake alizinduka.

“Kutokana na baridi kali ya chumba cha kuhifadhia maiti, mtoto wangu alipoingizwa mle ndani alipumua na hivyo kuhamishiwa ICU,” alisema Chalo.

Post a Comment