Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya CCM Lumumba
jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman
Kinana, alisema Nape ataendelea kuwa na wadhifa wa Katibu wa Itikadi na
Uenezi, lakini shughuli za usemaji wa chama zitafanywa na Sendeka.
“Kwa taratibu zetu, Mtendaji wa Chama anapoteuliwa kwenye majukumu
mengine, anatakiwa kuachia ngazi. Hivyo tumemchagua Ole Sendeka kuwa
Msemaji. Uteuzi wa Nape uko katika Halmashauri Kuu, hivyo utenguzi wake
utasubiri vikao hivyo vitakavyokaa hivi karibuni,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kinana alisisitiza kuwa Mwenyekiti wa chama
hicho, Jakaya Kikwete, atakabidhi kijiti cha uongozi kwa Dk. John
Magufuli, Juni, mwaka huu baada ya kuridhia kubeba majukumu hayo.
Kwa upande wake, Sendeka alimpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza
kwa vitendo kauli ya Hapa Kazi tu, na kwamba umejidhihirisha katika
kipindi kifupi cha uongozi kwa kudhibiti rushwa, ufisadi na ubadhirifu
wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka na ukwepaji kodi na matokeo
yake yanaoonekana.
“…matokeo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya
serikali ambayo yameiongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi kujikwamua na
umaskini kwa ustawi wa jamii kwa ujumla,” alisema.
Aidha, alisema CCM inamuunga mkono Rais Magufuli kwa hatua zozote
anazozichukua katika kurudisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa
umma na kwa walioguswa kwa namna moja au nyingine, wamefanyiwa kwa
kuzingatia sheria na misingi ya utawala bora.
Kuhusu kupokea wanachama waliokihama chama hicho na kurudi, Kinana
alisema wataweka utaratibu wa kuwachuja wale ambao waliondoka bila kutoa
lugha za matusi, kejeli na kashfa nyingine na maslahi binafsi, kwa
waliotenda hayo watafikiriwa na kwamba maoni ya wanachama yamepokelewa
na yatafanyiwa kazi.
Post a Comment