Wakati
Taifa likisubiri uteuzi wa wakuu wa wilaya huku wanaoshikilia nafasi
hizo wakiwa katika chekeche kwa kuzingatia vigezo vitano, Mkuu wa Wilaya
Iramba, mkoani Singida, Lucy Mayenga amemuomba Rais John Magufuli
asimjumuishe kwenye orodha ya wakuu hao anayotarajia kuitangaza wakati
wowote.
Rais
Magufuli ameweka bayana vigezo atakavyotumia kufanya uteuzi wa wakuu
hao wa wilaya ambavyo ni pamoja na suala la migogoro ya ardhi, tatizo la
elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu alivyovitangaza wakati akizungumza na wazee wa Dar es
Salaam na katika uteuzi wa wakuu wa mikoa, alizungumzia pia suala la
wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya wahusika
kuchukua hatua kudhibiti.
Akizungumza
kwenye kikao cha UWT, Mkoa wa Shinyanga mwishoni mwa wiki, Mayenga
ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu alisema aliwasilisha ombi hilo
binafsi kwa Rais Magufuli ili apate fursa ya kusimamia biashara zake
alizosema zinazodorora kutokana na kubanwa na majukumu ya ukuu wa
wilaya.
“Pamoja
na ukuu wa wilaya, mimi pia ni mbunge na wakati huohuo ni
mfanyabiashara; haya ni majukumu mengi kutekelezwa na mtu mmoja kwa
wakati moja,”alisema Mayenga
Aliwaambia
wajumbe waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika Kata ya
Nyamilangano, wilayani Ushetu kuwa biashara zake nyingi zilizopo mkoani
Shinyanga zimedorora kutokana na kukosa usimamizi wake.
“Ombi
hili nililitoa binafsi kwa Waziri Mkuu ambaye alinishauri kusubiri
uteuzi; isitafsiriwe kwamba nimeogopa kasi ya utendaji ya Serikali ya
Awamu ya Tano.Hapana! Nimeona ni vyema nibaki na ubunge na biashara
zangu,” alisema Mayenga ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Baadhi
ya wanachama wa UWT waliohudhuria mkutano huo walimpongeza kwa uamuzi
huo wakisema unapaswa kuigwa na viongozi wengine wenye majukumu mengi
kwa kuachia watu wengine nafasi za kutumikia umma badala ya
kung’ang’ania nafasi zote.
“Nampongeza
Mheshimiwa Mayenga kwa uamuzi wake wa kuomba asiteuliwe tena kwenye
nafasi ya ukuu wa wilaya kwa sababu itatoa fursa kwa watu wengine
kutumikia nafasi hiyo,” alisema Selina Mkula.
Katika
mkutano huo ambao Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa alitoa msaada wa
mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za
msingi Nyamilangano na Mitonga pamoja na Shule ya Sekondari Kisuke,
wanachama wapya 55 walijiunga na UWT.
Mbunge
huyo pia aliahidi kutoa vyerehani 20 kwa makatibu kata wa UWT ili
kusaidia harakati za maendeleo ya wananchi kwa kuanzisha vikundi vya
kiuchumi katika kata zao.
Post a Comment