Aliekuwa  Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka wananchi kulinganisha ahadi za Rais, Dk. John Magufuli  na CCM kuhusu elimu.
 
Ameyasema hayo siku mbili baada ya Dk.   Magufuli, aagize watendaji wa serikali kushughulikia utekelezaji wa sera yake ya kutoa elimu bure kuanzia  Januari mwakani.
 
Lowassa, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliahidi kutoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu.
 
Pia alikuwa ameahidi  kufuta michango yote  wanayotozwa wanafunzi, kama angepata ushindi wa kuwa rais.
 
Dk. Magufuli ambaye alikuwa akipeperusha bendera ya CCM, aliahidi kutoa elimu bure hadi kidato cha nne.
 
Taarifa   iliyotolewa jana na ofisi binafsi ya Lowassa, ilisema ahadi ya elimu bure aliyokuwa akiinadi, ilikuwa iwaguse hata wanafunzi ambao tayari wako shuleni na siyo wanaotarajiwa kuanza  mwakani pekee.
 
“Niliahidi watoto wote walioko na watakaoanza shule kuanzia kindergarten (shule ya awali) hadi chuo Kikuu serikali yetu ingegharimia.
 
“Na nilitangaza kufuta michango yote shuleni  kumpunguzia mzigo mwananchi,” taarifa hiyo ilimnukuu Lowassa akisema.
 
Taarifa hiyo ilisema   ahadi ya Dk. Magufuli,  “ni kwamba kuanzia Januari hakuna mtoto atakayelipa ada lakini hajatamka mustakhabali wa wanafuzi walioko shuleni kama wataguswa na hatua hiyo au laa.”
 
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, taarifa hiyo ilisema, Chadema kupitia Lowassa kilikwisha kuahidi kuwa elimu ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
 
“Vijana hawa wanahangaika na mikopo nasikia ni asilimia 17 tu kati ya wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata mikopo."

Post a Comment