Serikali imesema kuanzia sasa mtumishi wa umma atakayeshindwa kusimamia rasilimali za umma, achague moja kati ya mawili, kuacha kazi au atumbuliwe.


Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati alipozindua kitabu cha mwongozo wa usimamizi wa rasilimali za umma unaolenga kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa na kusimamiwa vizuri kwa maslahi ya Taifa.

Dk Mpango alizindua kitabu hicho jana katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma na baadaye semina elekezi iliyoandaliwa na Tume ya Mipango ilitolewa kwa watumishi wa Serikali.

Akizindua kitabu hicho, Dk Mpango alisisitiza kuwa mtumishi atakayeshindwa kuendana na maelekezo hayo ‘atatumbuliwa’.

“Mkishindwa kusimamia miradi kuna mawili, muache kazi mapema kama hamuwezi usimamizi au tuwatumbue, katika hilo hatutasita,” alisema

Katika ufafanuzi wake, Dk Mpango alisema katika bajeti ya Serikali mwaka 2016/17, fedha za maendeleo zilizotengwa ni asilimia 40 ya bajeti yote, hivyo lazima iwekwe mikakati ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inasimamiwa kabla na baada ya kukamilika.

“Kwenye masoko ya fedha na mitaji zipo fedha nyingi, lakini ili mwekezaji awekeze kwenye mradi ni lazima mradi husika uwe umeandaliwa vyema,”

“Hapa nchini kwetu tumekuwa na tatizo la muda mrefu la kuwa na miradi ambayo haijaandaliwa vizuri kwa hiyo tunakosa fursa ya kufikia masoko ya mitaji,” alisema Dk Mpango.

Alisema kitabu hicho ni muongozo wa wataalamu na wadau wote ili kuiwezesha nchi kuandaa miradi mizuri, kufuatilia utekelezaji wake ili iweze kuwasaidia wananchi.

“Haiwezekani tuendelee kulima mahindi na kuuza mazao hayo bila kuyaongezea thamani, haiwezekani watu wachukue dhahabu na sisi kubaki na mashimo,” alisema.

Dk Mpango aliwaonya watumishi umma waliokuwa katika uzinduzi huo kwamba kuanzia sasa wana dhamana kubwa kwa Watanzania kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuweka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo inazaa matunda.

Alisema Tanzania inaweza kuwa nchi ya kipato cha kati kabla ya 2025 kama miradi yote itasimamiwa vizuri.

“Ili nchi yetu iweze kubadilika na rasilimali ziwasaidie wananchi wetu ambao bado ni masikini, jambo muhimu ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa vizuri. Ili itekelezwe vizuri lazima iandaliwe vizuri na isimamiwe vizuri hilo limekuwa tatizo letu la muda mrefu,”alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri alisema lengo la semina hiyo ambayo iliwashirikisha wataalamu kutoka wizara mbalimbali, Idara na Halmashari ni kuwajengea uwezo wa kutambua kipi wanapaswa kukifanya.

“Lazima wataalamu hawa ambao ndiyo wanapanga na kuisimamia miradi hiyo wajue kipi wanapaswa kukifanya, Serikali mwaka ujao wa fedha asilimia 40 zimepangwa kupelekwa katika miradi ya maendeleo sasa tukiwajengea uwezo wataweza kuisimamia vyema na kupanga miradi yenye tija,”

“Wafadhili wa miradi ya maendeleo wapo wengi, lakini tulikuwa tunashindwa kuisimamia kwani hapakuwa na mipango na usimamizi mzuri, lakini Serikali ya Rais Magufuli ambayo imeelekeza nguvu katika miradi ya maendeleo bila shaka itawashughulikia watakaoshindwa kwenda na kasi.” alisema Mwanri.

Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Wilhem Ngasamiaku alisema baadhi ya miradi inashindwa kutekelezwa kwa ufanisi kutokana na wasimamizi kutokuwa na uelewa wa kutosha.

Alisema kufanyika kwa semina hiyo sambamba na maelekezo yaliyopo katika kitabu hicho, yatasaidia kuwawezesha wataalamu wa usimamizi wa miradi hiyo kuwa na uelewa na jinsi ya kutoa kipaumbele, kuisimamia ili iwe na ufanisi.

Post a Comment